Pinda: Haikubaliki kanda ya ziwa kuwa na utapiamlo

Muktasari:

Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mizengo Pinda amewataka viongozi na wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kujitafakari na kurekebisha kasoro zinazofanya mikoa hiyo kuwa na tatizo la utapiamlo licha ya kuwa na wingi wa chakula

Bariadi. Katika ulingo wa kisiasa nchini Tanzania, mikoa ya Kanda ya Ziwa ndiyo huaminika kuamua matokeo kwenye uchaguzi wa nafasi ya urais kutokana na wingi wa  wapiga kura.

Hii ni kutokana na kanda hiyo inayoundwa na mikoa ya Mara, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Shinyanga kuwa na theluthi moja ya idadi ya watu Tanzania.

Hata hivyo, Kanda ya Ziwa ni kati ya maeneo Tanzania yanayokabiliwa na tatizo la utapiamlo, umaskini wa kipato miongoni mwa wakazi na mwamko mdogo kielimu.

Kutokana na ukweli huo, Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mizengo Pinda amewataka viongozi na wakazi wa mikoa hiyo kujitafakari ni wapi walipokea na kurekebisha kasoro hizo.

"Theluthi moja ya Watanzania wanatoka Kanda ya Ziwa ambayo pia imejaaliwa rasilimali nyingi. Lakini eneo hili bado ni kati ya maeneo nchini yenye utapiamlo. Hii haikubaliki na lazima tujiulize tulipokosea na kujirekebisha," amesema Pinda leo Jumanne Agosti 6, 2019 katika maonyesho ya nanenae yanayoendelea Bariadi mkoani Simiyu.

"Kanda ya Ziwa ndiyo kinara kwenye kilimo cha pamba na mpunga. Ndiyo inaongoza kwa wingi wa mifugo mingi na shughuli za uvuvi. Haiwezi kuilinganisha na kanda zingine kwa wingi wa rasilimali; lakini bado kuna umaskini. Haikubaliki," ameongeza

Akifafanua, waziri mkuu huyo mstaafu amesema licha ya mikoa hiyo kuwa na wingi wa chakuka ikiwemo mazao, nyama na samaki, mfumo wa ukuaji bado unawafanya wakazi wake kuwa na utapiamlo.

"Kuna wakati utafiti ulitaja mikoa ya Rukwa na Katavi kuwa miongoni mwa maeneo yenye utapiamlo. Watu kule walichachamaa wakisema wao ndio wanaongoza kwa uzalishaji wa mahindi; lakini suala siyo uwingi wa chakuka, bali namna ya ulaji," amesema Pinda