Nyalandu asema ni aibu kwa Tanzania Lissu kufutiwa ubunge

Waziri wa zamani wa maliasili na utalii nchini Tanzania, Lazaro Nyalandu

Muktasari:

  • Lazaro Nyalandu, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika serikali ya awamu ya nne nchini Tanzania amesikitishwa na kushangazwa na uamuzi uliotolewa jana na Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai baada ya kutangaza kuwa Tundu Lissu si mbunge kwani amekosa sifa za kuwatumikia wananchi wa Singida Mashariki.

Dar es Salaam. Waziri wa zamani wa maliasili na utalii nchini Tanzania, Lazaro Nyalandu amesema uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai wa kutangaza kiti cha ubunge wa Singida Mashariki kilichokuwa kikiongozwa Tundu Lissu kiko wazi.

Spika Ndugai alitangaza uamuzi huo jana bungeni akisema hafahamu mbunge huyo aliko na hajajaza fomu za madeni na mali za viongozi wa umma.

Nyalandu ambaye alikuwa mbunge wa Singida Kaskazini kupitia CCM alijiuzulu ubunge na kuhamia Chadema Oktoba 30 mwaka 2017. Katika ukurasa wake wa akaunti ya Twitter aliandika maandiko mbalimbali kuhusu Lissu kupoteza ubunge wake.

“Kitendo cha Mh. Spika kumvua Ubunge Mh. @tundulisu huku akiwa anaendelea na matibabu Ubelgiji kufuatia shambulio dhidi yake la kupigwa risasi ni aibu na fedheha kwa demokrasia. Tundu Lissu ameonewa sana, haipendezi kuendelea kumuumiza zaidi. Hakika haki huinua Taifa. #BungeTZ.”

Ujumbe mwingine wa Nyalandu ulisema, “Mbunge wetu #SingidaMashariki. #TunduLissu. Tunaendelea kukuombea kaka. Tunakupenda sana. Mungu aendelee kukulinda. Karibu nyumbani, tunakusubiri kwa shauku mwezi Septemba.”

Katika ukurasa huo, Nyalandu ameweka kipande cha video na ujumbe unaomnukuu Spika Ndugai kwa kauli mbili tofauti zinazokinzana, ikiwamo inayowatia moyo wapiga kura wa Lissu wa Singida Mashariki, ikimnukuu Ndigai akitoa kauli hiyo Septemba 7 mwaka 2017 siku aliyoshambuliwa kwa risasi akisema: "Mimi ninawahakikishia wananchi hasa wapiga kura wake, mgonjwa (Lissu) yupo mikono salama."

Hata hivyo, kauli nyingine aliyoambatisha ni ile aliyoitoa Spika Ndugai jana wakati akitangaza kufuta ubunge wa Lissu: "Lissu hayupo bungeni, hospitalini, na taarifa zake spika hana kabisa, nimemwandikia mwenyekiti wa @TumeYaUchaguzi kuwa jimbo la Singida Mashariki kipo wazi."