Nape mwenyekiti wa tatu kamati za Bunge kujiuzulu

Muktasari:

Ofisi ya Spika wa Bunge la Tanzania imethibitisha kupokea barua ya mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye ya kujiuzulu nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye aliyejiuzulu uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii amekuwa mwenyekiti wa tatu kuachia ngazi baada ya Hawa Ghasia kufanya hivyo kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti, mwaka jana, na mwenyekiti wa kamati ya Bunge wa kwanza kujiuzulu alikuwa ni Dk Dalali Kafumu wa viwanda, biashara pamoja na makamu wake, Vick Kamata.

Nape ambaye amewahi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alijiuzulu uenyekiti huo jana jioni wakati kamati aliyokuwa anaiongoza inawasilisha taarifa yake ya mwaka 2018 bungeni jijini Dodoma.

Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai alithibitisha taarifa hiyo jana usiku alipozungumza na Mwananchi kwa simu kutoka mjini Dodoma.

“Ni kweli na mimi barua nimeiona,” alisema Kagaigai

Mwananchi lilipotaka kujua sababu za Nape kujiuzulu,  Kagaigai alisema, “anataka ku-concetrate kwenye ubunge wake.” 

Ghasia na Nape ambao ni wabunge kutoka mikoa ya Kusini wanakumbukwa jinsi walivyolitikisa Bunge kutokana na sakata la korosho mwaka jana, jambo ambalo lilifanya Serikali kuingilia kati na kwenda kununua korosho kwa wakulima.

Mchakato huo wa ununuzi wa korosho unaendelea mpaka sasa..