VIDEO: Mwalimu aliyemchapa mwanafunzi hadi kufa alivyozimia mahakamani baada ya kuhukumiwa kunyongwa

Muktasari:

Kesi dhidi ya walimu hao imeendeshwa ndani ya siku thelathini na kutolewa hukumu na Jaji Lameck Mlacha


Bukoba. Wakati mwalimu Respicius Mtazangira akianguka kizimbani baada ya kuhukumiwa kifo kwa mauaji ya mwanafunzi, mshtakiwa mwenzake Heriet Gerald ameachiwa na Mahakama Kuu.

Baada ya kuanguka kizimba kilizungukwa na askari na watu kuambiwa watoke nje ya ukumbi wa Mahakama, lakini baadaye alipitishwa mlango wa nyuma na kuwaacha solemba mamia ya wananchi waliokuwa wanasubiri kumuona.

Hukumu hiyo imesomwa leo Machi 6, 2019 na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Lameck Mlacha.

Washtakiwa wote walishtakiwa kwa kosa la mauaji ya makusudi ya mwanafunzi Sperius Eradius wa Shule ya Msingi Kibeta iliyopo mkoani Kagera.

Katika hukumu iliyosomwa kwa saa mbili, Jaji Mlacha amesema upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha ushiriki wa Heriet kwenye kifo cha Sperius, huku Respicius akitiwa hatiani na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Kuhusu nia ya kuua, Jaji Mlacha amesema Mwalimu Respicius ambaye alikuwa akisimamia nidhamu, alimpiga kwa fimbo ya kawaida mwanafunzi huyo na baadaye kutumia kuni, jambo lililosababisha majeraha kwenye mwili wa mwanafunzi huyo na ni ushahidi kuwa alipigwa mara nyingi.

Mgongano wa mashahidi kuhusu uhusika wa Heriet huku wakitofautiana idadi ya viboko umetoa faida kwa  mshtakiwa hiyo kuonekana kuwa ushahidi uliotiliwa shaka na Mahakama.

Katika kesi hiyo namba 56/2018, Mahakama imezingatia ushahidi wa daktari wa magonjwa na vifo kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza, Kahima Jackson ambaye alisema kifo kilisababishwa na mshtuko uliotokana na kipigo.

Wakili Mkuu wa Serikali, Hashimu Ngole akijibu kuhusu kuwahi kumalizika kwa kesi hiyo ikilinganishwa na nyingine za mauaji, amesema ilikuwa na masilahi ya umma na walipeleka ombi maalumu kutaka ipewe kipaumbele na kwamba, hawana mpango wa kukata rufaa kwa mshtakiwa aliyeachiwa huru

Wakili wa washtakiwa aliyewaongoza wengine wanne kupangua shtaka dhidi ya watuhumiwa, Aaron Kabunga amesema Mahakama imefanya kazi yake na wameridhika na hukumu.