Membe azungumzia Lissu kupoteza ubunge

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje nchini Tanzania, Bernard Membe

Muktasari:

  • Waziri wa zamani wa mambo ya nje na Mbunge wa Mtama (CCM), Bernard Membe ameshangazwa na hatua ya Spika wa Bunge la nchi hiyo, Job Ndugai kusema Tundu Lissu amepoteza sifa za kuwa mbunge.

Dar es Salaam.  Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje nchini Tanzania, Bernard Membe ameshangazwa na uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kusema Tundu Lissu amepoteza sifa ya kuendelea kuwa mbunge wa Singida Mashariki.

Juni 28, 2019, Spika Ndugai alisema Lissu amepoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na sababu mbili ambazo ni kutokujaza fomu za mali na madeni za viongozi wa umma pamoja na kutokutoa taarifa kwake (spika) kwamba yuko wapi.

Akizungumzia  hatua hiyo leo Jumanne Julai 2, 2019 nje ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Membe aliyeulizwa na waandishi maoni yake juu ya suala la Lissu kupoteza sifa ya kuendelea kuwa mbunge amesema;

“Kama Mtanzania na mimi nilishangazwa, sasa tusubiri Lissu aje, nina uhakika kabisa kuwa ataenda mahakamani na kama kuna haki ataipata mahakamani,” amesema mwanadiplomasia huyo

Kuhusu matukio ya utekaji, Membe ametoa wito kwa viongozi mbalimbali waliopo madarakani na wastaafu, wakubwa kwa wadogo kujitokeza kukemea vitendo hivyo ambavyo amesema kama havitakemewa kwa pamoja havileti picha nzuri kuelekea uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020.