Mbunge CCM atoa angalizo utekelezaji miradi mikubwa

Mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mbunge wa Igunga (CCM), Dk Dalaly Kafumu ameishauri Serikali ya Tanzania kutafuta mikopo yenye riba nafuu kukamilisha miradi mikubwa ukiwemo wa reli ya kisasa (SGR) kwa kuwa kutumia fedha zake miradi hiyo itachelewa kukamilika.


Dodoma. Mbunge wa Igunga (CCM), Dk Dalaly Kafumo ameishauri Serikali ya Tanzania kutafuta mikopo yenye riba nafuu ili kukamilisha haraka ujenzi wa miradi mikubwa, akitolea mfano reli ya kisasa (SGR).

Amesema uamuzi wa Serikali ya Tanzania kutumia fedha yake yenyewe katika ujenzi huo kutasababisha mingi ichelewe kukamilika.

Dk Kafumo alitoa kauli hiyo jana jioni Jumatano Juni 19, 2019 katika mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2019/2020. 

“Tumeamua kujenga miundombinu ili kujenga uchumi wetu tuna miradi ya umeme, barabara, reli na ununuzi wa ndege.”

“Ili ujenge uchumi wako lazima uwe na miundombinu na tumefanya vizuri sana. Kama nilivyosema kuna changamoto kadhaa kama fedha. Ni vizuri tukaishauri serikali itafute utaratibu wa kupata fedha ili miradi hii iende haraka,” alisema Dk Kafumo.

Alisema kama Serikali ya Tanzania itaamua kutumia fedha zake katika ujenzi wa miradi hiyo itachukua muda mrefu kukamilika na kuchelewesha ukuaji wa uchumi.

"Dk Mpango (Philip-Waziri wa Fedha na Mipango) nashauri kwa namna fulani tutafute fedha kwa maana ya mikopo yenye gharama nafuu. Twende huko tuangalie tutawezaje kujenga reli kufika Kigoma kwa kipindi cha miaka 10 au mitano ili ianze kuleta faida.”

“Tukifanya hivi tunavyofanya nachelea kusema mpaka 2025 bado tutakuwa tumeishia Tabora na hali itakuwa ngumu maana tutaanza kulipa mikopo wakati hatujaanza kuzalisha,” alisema.