Mapendekezo marekebisho ya sheria yaziweka kikaangoni kampuni, NGO

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania imewasilishwa muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2019 ambao pamoja na mambo mengine umeongeza masharti katika usajili wa kampuni na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO)

Dodoma. Serikali ya Tanzania imependekeza kampuni zilizosajiliwa chini ya sheria ya kampuni ambazo zinajishughulisha  na shughuli za kijamii ndani ya miezi miwili tangu kuanza kwa marekebisho ya sheria hiyo, kujisajili chini ya sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO).

Ikiwa jambo hilo halitatekelezwa, inapendekezwa kuongeza kifungu kipya cha 400A kwa lengo la kumpa msajili wa kampuni mamlaka ya kufuta kampuni yoyote pale itakapoonekana  inajihusisha na masuala ya kijinai au masuala yaliyozuiwa, mamlaka hayo yataambana na tahadhari za kisheria kulinda kampuni husika.

Pia, mkurugenzi wa uratibu wa NGO amepewa mamlaka ya kufuta usajili wa shirika lolote ambalo halikidhi masharti ya usajili.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Juni 27, 2019 na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ya Tanzania, Profesa Adelardus Kilangi wakati akiwasilisha bungeni jijini Dodoma muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2019.

Muswada huo unapendekeza marekebisho katika sheria nane ambazo ni Sheria ya Makampuni (sura ya 212), Sheria ya Hakimiliki (sura ya 218), Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza (sura ya 230), Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali (sura ya 56), Sheria ya Vyama vya Kijamii (Sura ya 337), Sheria ya Takwimu (sura ya 351), Sheria ya Uwakala wa Meli (sura ya 415) na Sheria ya Muunganisho wa Wadhamini (sura ya 318).

“Lengo la marekebisho haya ni kutofautisha usajili wa kampuni na mashirika yasiyo ya kiserikali na kampuni, aidha inapendekeza kurekebisha kifungu cha 32(1) kwa lengo la kuondoa mgongano wa usajili uliopo kati ya msajili wa kampuni chini ya sheria ya kampuni na msajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO),”amesema Profesa Kilangi.

 

Kuhusu NGO

Profesa Kilangi amesema marekebisho ya kifungu cha nne yanalenga kupanua wigo wa majukumu na wajibu wa mkurugenzi wa uratibu wa Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO), ili kumwezesha kuzuia NGO kutekeleza majukumu yake endapo yatakuwa kinyume na sheria na kutathmini shughuli zinazotekelezwa na mashirika hayo.

“Kifungu kipya cha 4A kinampa msajili mamlaka ya kufanya uchunguzi wa mwenendo wa shirika lolote lililo chini yake. Kifungu cha 8A kinaongezwa kwa kuweka masharti ya kufuta usajili wa shirika lisilo la kiserikali ambalo halikidhi masharti ya usajili.”

“Marekebisho ya kifungu cha 17 yanalenga kuweka ukomo wa vyeti vya usajili na utaratibu wa kuhuisha vyeti hivyo kila baada ya kipindi cha miaka 10. Marekebisho ya kifungu cha 31 yanaweka masharti kuhakikisha kwamba mashirika yasiyo ya kiserikali yanafuata kanuni za fedha za uwazi na uwajibikaji.”

 

Filamu

Kuhusu utengenezaji wa filamu, Profesa Kilangi amesema mtu au kampuni ya kigeni inayotaka kutumia eneo lolote la Tanzania kutengeneza filamu nchini, anapaswa kuwasilisha nakala ya awali iliyotumika kutengeneza filamu husika, kubainisha maeneo ya Tanzania ambayo yatatumika katika kuandaa filamu husika.

“Pia kuwasilisha kwa bodi ya filamu nakala ya filamu iliyotengenezwa na kuruhusu filamu au kipande cha picha jongevu kutumiwa na Serikali ya Tanzania kutangaza maliasili na utalii, mila na tamaduni za Mtanzania.”

“Aidha mtu au kampuni hiyo itatakiwa kubainisha maeneo ya nchi yanayofaa kwa ajili ya utayarishaji wa filamu pamoja na kujaza fomu maalum kabla ya kuondoka nchini. Kifungu hiki kinaweka adhabu kwa mtu atakayekiuka masharti hayo,” amesema Profesa Kilangi.

Mapendekezo hayo yameongeza kifungu kipya kinachomtaka mtu au kampuni ya filamu ya kigeni kuwasilisha sehemu ya faida itokanayo na kazi za filamu zinazotayarishwa nchini.