VIDEO: Ma RC-DC wanaowaweka watu ndani kikaangoni

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Kapteni mstaafu George Mkuchika amesema wakuu wa mikoa na wilaya watakaowaweka watu ndani bila kuzingatia sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1984 watashtakiwa wao binafsi na watu waliowaweka ndani, hawatatetewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Kapteni mstaafu George Mkuchika amesema wakuu wa mikoa (RC) na wilaya (DC) watakaowaweka watu ndani kinyume cha sheria watashtakiwa wao binafsi.

“Hawatatetewa na  Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Ninamshukuru mwanasheria mkuu wa Serikali ametoa waraka kwa wote waliopewa mamlaka ya kuweka mtu ndani na mimi kanipa nakala, ikieleza mazingira ya mtu kuwekwa ndani,” amesema Mkuchika leo Jumatatu Aprili 15, 2019 bungeni jijini Dodoma.

Akiwa anajibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti hiyo mwaka 2019/2020 inayotarajiwa kupitishwa leo jioni, Mkuchika amesema, “Moja awe ametenda kosa la jinai, na (mkuu wa wilaya, mkoa) uweke kwa maandishi kwa nini umemuweka ndani. Utawala bora unasema kesi ikiwa mahakamani hakuna mkuu wa wilaya, mkoa au waziri anayeweza kuisikiliza.”

“Mahakama ya chini uamuzi wake unaweza kutenguliwa na mahakama ya juu wengine wamejiingiza katika matatizo kwa mambo ambayo tayari yametolewa hukumu mahakamani.”

Mkuchika amesema wakuu wa wilaya na mikoa wanapotumia mamlaka yao kuweka mtu mahabusu kwa saa 24 na 48 wazingatie sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997.

“Sheria hii inawapa mamlaka kuwaweka ndani watu pale inapothibitika anahatarisha amani. Nawaomba wabunge tusikilize sheria na nawaomba na huko walipo (wakuu wa wilaya na mikoa) wanisikilize,” amesema.

“Mtu anawekwa ndani kama amehatarisha amani, si watu wanadaiana madeni hawataki kulipa unawapeleka kwa mkuu wa mkoa, hawa wanadaiana si kuhatarisha amani.”

Alisema viongozi hao wakitekeleza hatua kinyume na utaratibu wanaweza kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kushtakiwa binafsi.

“Tumekemea hili jambo mwanasheria wa Serikali hatomtetea mtu aliyevunja sheria makusudi kumuweka mtu ndani bila sababu. Utapelekwa mahakamani na huyo uliyemuweka ndani na mwanasheria mkuu wa Serikali hatokuja kukutetea,” amesisitiza.