VIDEO: Lukuvi awasilisha bajeti yake, atoa agizo kwa Ma RC, DC

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi akijiandaa kusoma hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020, bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amewasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2019/20 ya Sh62.68 bilioni. Mwaka wa fedha 2018/19 ilitengewa Sh65.98 bilioni

Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewataka wakuu wa mikoa (RC) na wilaya (DC) kuhakikisha wanatatua migogoro ya ardhi kabla ya uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba 2019.

Waziri Lukuvi ametoa agizo hilo leo Ijumaa Mei 31,2019  bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2019/20 ya Sh62.68 bilioni.

Amesema katika mwaka wa fedha 2019/20, wizara itaendelea kutatua migogoro ya mipaka ya ndani ya nchi kwa kadri itakavyokuwa inajitokeza.

“Natoa rai kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuendelea kubaini na kutatua migogoro ya mipaka ya vijiji na wilaya kabla ya uchaguzi ujao wa serikali za mitaa,” amesema Waziri Lukuvi

Waziri huyo amesema katika mwaka 2019/, wizara inakusudia kusajili hatimiliki na nyaraka za kisheria 152,000. Kati hizi, hati za kumiliki ardhi ni 100,000, hati za kumiliki sehemu ya jengo/ eneo 2,000 na nyaraka za kisheria 50,000.

“Napenda kutumia fursa hii kuhimiza wananchi kuona umuhimu wa kusajili nyaraka mbalimbali zinazotokana na miamala ya ardhi iliyosajiliwa, mfano mikataba ya uhamisho wa miliki, wosia, rehani za mikopo nk. Hii itasaidia kuwaepusha na wimbi la utapeli wa ardhi,” amesema Mbunge huyo wa Isimani (CCM)

Amesema mwaka 2019/20 wizara yake kwa kushirikiana na mamlaka za upimaji nchini itaandaa na kusajili vyeti vya ardhi ya Kijiji 100 kati ya 1,392 ambavyo havijasajiliwa na hati za kimila 150,000 zitaandaliwa.

Waziri Lukuvi amesema wizara hiyo imepanga kusajili nyaraka za kisheria zipatazo 53,000.

“Natoa rai kwa mamlaka za upangaji nchini kuhakikisha zinamilikisha viwanja vyote vilivyopimwa ili wananchi waweze kuwa na miliki salama. Pia, nawahimiza wamiliki wote wa ardhi kuchukua hati zao zilizokamilika kutoka ofisi za msajili wa hati zilizopo katika ofisi za ardhi za kanda,” amesema