Kiongozi Mwenge wa Uhuru agoma kuzindua miradi ya maji, barabara

Askari wa kikosi cha kuzuia fujo (FFU) wakibandua kibao kilichowekwa kwaajili ya ufunguzi wa daraja la mto Mara katika kijiji cha Kiterere wilayani Tarime baada ya kiongozi wa mbio za mwenge kukataa kuzindua mradi huo. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Mbio za mwenge wa Uhuru mwaka 2019 zimekataa kuzindua miradi miwili katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.


Tarime.  Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Mzee Mkongea amekataa kuzindua miradi miwili ya sekta ya maji na barabara Wilaya ya Tarime mkoani Mara kutokana na kutokukidhi vigezo.

Katika mbio za Mwenge mwaka jana, aliyekuwa kiongozi wake, Charles Kabeho ambaye sasa ni mkuu wa wilaya hiyo, pia alikataa miradi  kadhaa kwa kile alichodai ilitekelezwa chini ya kiwango.

Jana, Jumatatu Juni 3, 2019 Mwenge wa Uhuru umeingia katika Wilaya ya Tarime inayoongozwa na Kabeho.

Akizungumza katika mradi wa kwanza wa maji Mtaa wa Gamasara, Mkongea amesema mbio za Mwenge haziwezi kuukubali mradi huo kutokana na kutokukidhi vigezo.

Amesema miongoni mwa kasoro walizozigundua baada ya kufanya ukaguzi katika mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh484.9 milioni ni nondo zilizotumika katika ujenzi huo kutopimwa.

"Nondo zilitakiwa kupimwa kitaalamu na taarifa iwepo lakini hapa hicho kitu hakijafanyika, hivyo kwa vile ujenzi bado unaendelea, mkuu wa wilaya (Kabeho) nakuagiza kusimamia upimaji huo  na tupate taarifa ndani ya wiki mbili kuanzia sasa," amesema Mkongea.

Kuhusu mradi wa daraja katika Kijiji cha Kiterere, kiongozi huyo amesema Mwenge huo hauwezi kuzindua daraja hilo kutokana na kasoro mbalimbali ikiwamo ukosefu wa alama za barabarani.

"Hapa tumekuja kuzindua maana yake ujenzi umekamilika, hivyo kutokana na kasoro tulizozigundua nakuagiza mkuu wa wilaya (Kabeho) kwa mamlaka uliyonayo kuhakikisha kasoro hizo zinarekebishwa ndio nitakuja kuzindua mradi huu," amesema Mkongea.

Akizungumza baada ya miradi hiyo kukataliwa, Kabeho amesema amepokea maelekezo hayo na atafanyiwa kazi ndani ya muda mfupi.