Chadema yaendelea kulia na ubunge wa Lissu

Katibu Mkuu Chadema, Dk Vincent Mashinji akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alipokuwa akitoa tamko la chama hicho kufuatia spika wa bunge, Job Ndugai kutangaza kiti cha ubunge wa Singida Mashariki kilichokuwa chini ya Tundu Lisu kuwa wazi. Picha na Ericky Boniphace


Muktasari:

Baada ya Spika wa Bunge Job Ndugai kutangaza kiti cha ubunge wa Singida Mashariki kuwa wazi chadema kimesema kuna mchezo mchafu unaochezwa na Lissu alipaswa kusikilizwa kabla ya kuhukumiwa.

Dar es salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitendo cha Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kutangaza kiti cha ubunge wa Singida Mashariki kilichokuwa chini ya Tundu Lissu kuwa wazi ni mchezo mchafu unaochezwa.

Juni 28,2019, Ndugai alilieleza Bunge kuwa amemwandikia Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi kuwa jimbo la Singida Mashariki ambalo lilikuwa likiongozwa na Lissu sasa liko wazi. Hivi sasa Lissu yupo nchini Belgium akiendelea na matibabu baada ya kujeruhiwa na risasi, Septemba 7, 2017 Jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Juni 30, 2019, Katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amesema Lissu amehukumiwa bila kusikilizwa.

Amesema baada ya Lissu kushambuliwa, Spika aliwahi kusema atakwenda kumuona popote atakapokuwa akipatiwa matibabu lakini hakufanya hivyo.

“Spika Ndugai alishiriki kufika hospitali ya Dodoma na kushiriki vikao vingine vya maamuzi ya matibabu ya Lissu lakini leo anadiriki kusema hajui alipo,” amesema Mashinji.

Amesema ipo mamlaka ambayo ni sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma, haijawahi kupeleka wito wala taarifa kuhusiana na Lissu.

"Tume ya maadili ina adhabu zake kwa mujibu wa sheria ikiwemo kushushwa cheo, kuombwa kujiuzulu au kupewa adhabu yoyote kulingana na mazingira ya ofisi" amesema

Dk Mashinji ameongeza kuwa Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma inajua madhara ya kumuhukumu mtu

“Kwamujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 67 (2)d kinamnyima haki ya kugombea ubunge kwa kipindi cha miaka mitano,” ameongeza.