Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia tani milioni 25

Muktasari:
- Upanuzi wa gati namba moja hadi saba utasaidia bandari hiyo kuhudumia tani milioni 25 kutoka milioni 16.2 inayohudumia sasa
Dar es Salaam. Upanuzi na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam unaoendelea utakapokamilika utaifanya iweze kuhudumia tani milioni 25 badala ya milioni 16.2
Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Desemba 3 na mkurugenzi wa bandari hiyo, Fred Liundi alipkuwa akiwaeleza wanaabari juu ya maboresho ya bandari hiyo.
Amesema bandari ilifikia kiwango chake cha juu cha shehena kabla ya upanuzi kwa kuweza kuhudumia tani milioni 13.5 kiwango ambacho walikipita tangu mwaka 2015.
“Mwaka uliopita tulihudumia tani milioni 16.2 ambazo tutahudumia mwaka huu pia. Hii inamaanisha kuwa uhitaji wa kupanua bandari lilikuwa ni jambo la msingi,”amesema Liundi.
Amesema baada ya kumaliza upanuzi na uboreshaji wa bandari hiyo itaweza kuhudumia tani milioni 25.
Kwa upande wake mkurugenzi wa huduma za uhandisi wa Mamlaka ya Bandari(TPA), Charles Ogare amesema katika mradi huo wanaboresha gati namba moja hadi saba.
“Namba moja tunajenga nguzo sehemu ya kushushia magari na yadi ya kuweka magari katika eneo ambalo ni la maji lakini tumeshayatoa,”amesema.
Ogare amesema gati hiyo namba moja upanuzi wake utaisha wiki hii kwa kumaliziwa kuwekwa mipira minene ambayo meli huegemea inapotia nanga.
“Wiki hii Ijumaa meli zitaanza kutia nanga na kwa upande wa gati namba mbili itakabidhiwa mwezi Machi mwakani,”amesema Ogare.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko amesxemagati litakaloweza kuleta mabadiliko ni liloloitwa roro ambalo ni jipya wanaliita namba sifuri na limefikia asilimia 65 ya utekelezaji.
“Tulipata changamoto ya udongo lakini limeshaisha na gati hili lilikamilika mele yenye urefu wa mita 220 inaweza kushusha magari hata 3,000.”