Aliyesota miaka 20 jela aoa aliyehukumiwa kifungo cha maisha

Moshi. Mkazi wa Soweto mkoani Kilimanjaro aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia nguvu na kutumikia adhabu miaka 20, amesema kujua haki zake kulimsaidia apangue hukumu hiyo.

Mkazi huyo, Mohamed Abubakar Urotu pia alipata mwenza wakati akitumikia kifungo hicho baada ya kukutana na mfungwa aliyekumbwa na mkasa kama wake na sasa wanaishi kama mke na mume.

“Watanzania tujitahidi kujua haki zetu za msingi maana hata mimi ningejua haki zangu nisingefungwa kwa muda wote huo niliokaa gerezani,” alisema Urotu.

“Kitu ambacho sitasahau ni kwamba haki zinashindwa kupatikana kwa wakati. Mfano kama mimi nimepata haki yangu baada ya kumaliza miaka 20 jela, hivyo mtu anakosa haki kwa wakati na hii inasikitisha sana.”

Jaji Eusebia Munuo wa Mahalama Kuu alikubaliana na hukumu iliyompa Urotu (47) kifungo cha miaka 30 mwaka 1997 baada ya kumkuta na hatia katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia nguvu.

Lakini, katika mazungumzo na Mwananchi Ijumaa, Urotu alisema alipambana Mahakama ya Rufani na baadaye Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu iliyopo jijini Arusha ambayo ilibaini kuna haki hakuzipata.

Mwaka 2013 akiwa gerezani, Urotu alikata rufaa katika Mahakama Kuu kupinga hukumu iliyomtia hatiani, lakini akashindwa na baadaye kwenda Mahakama ya Rufani ambayo pia haikukubaliana na hoja zake.

Ndipo Urotu akaamua kukata rufaa nyingine katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu mwaka 2016, chombo hicho cha Umoja wa Afrika kikaja na uamuzi ambao ulitosha kumfanya awe huru.

“Lakini mahakama ya Tanzania ikapewa muda iangalie namna ya kuniachia. Niliachiwa Julai 28/2017,” alisema.

“Baada ya kuona nimeshinda nilipewa nafasi nyingine ya kuomba malipo (ya fidia) kwa vile mahakama za Tanzania zilifanya makosa katika hukumu,’’ alisema Urotu akizungumzia kuachiwa kwake.

“Niliomba tena msaada wa mawakili na mahakama iliona kuna haki ya kulipwa na Serikali ya Tanzania na jana (Alhamisi) nililipwa Sh2 milioni, mke wangu Sh1.5 milioni na mtoto wangu Sh1 milioni.”

Baada ya miaka 20 gerezani, maisha ya familia hayakuendelea kama alivyoyaacha. Mke na mtoto aliowaacha, walitoweka, lakini alikuwa na kitu cha kumfariji.

“Baada ya kutoka gerezani jamii iliyokuwa inanizunguka ilinipokea vizuri na kwa shangwe kwa kuwa niliishi nao vizuri,” alisema.

Na kikubwa zaidi ni mwenza aliyempata akiwa gerezani na ambaye alikuwa akipitia kipindi kigumu kama chake.

“Nikiwa gerezani nilikutana na dada aliyepitia shida kama zangu,” alisema.

Urotu alisema dada huyo anaitwa Rose Malle, alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la mauaji, lakini naye alikata rufaa mahakama hiyo ya Afrika ambayo ilimuachia huru baada ya kumuona hakuwa na hatia.

“Tulielewana sana (na Rose) na tukawa marafiki nikiwa naye gerezani,” alisema.

“Baada ya kufahamiana naye nikiwa gerezani (Isanga, Dodoma), mimi nilitangulia kutoka kutokana na mahakama kuniachia huru mwaka 2017.

“Huyu dada, ambaye sasa ndio mke, naye alikata rufaa akiwa gereza la Isanga Dodoma na baadaye alipokuja gereza la Kisongo, Arusha nilienda kumuona. Na siku hiyo nilimfuata mahakamani ambako aliachiwa huru nikiwepo baada ya kushinda ile rufaa. Baada ya hapo nilianza kuishi naye kama mke wangu na taratibu nyingine ziliendelea.”

Alisema sasa anamshukuru Mungu kwa kuwa mambo yake yanaenda vizuri.

“Namshukuru Mungu kwa kunikutanisha na mwanamke huyu kimaajabu,” alisema Urotu.

“Na sasa tunaishi kama mume na mke na tuna mtoto mmoja licha ya changamoto nilizopitia baada ya familia yangu yote niliyokuwa naishi nayo kusambaratika. Wakati nafungwa niliacha mke na mtoto mmoja.”