Waziri agoma kufungua mgodi

Muktasari:

Waziri wa madini, Dotto Biteko amesema hatafungua mgodi wa madini wa Nyarugusu hadi pale wamiliki watakapotimiza masharti waliyopewa pamoja na kurudisha dhahabu walizotorosha Oktoba mwaka jana

Geita. Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema Serikali haipo tayari kufungua mgodi wa dhahabu wa Nyarugusu uliopo kata ya Nyarugusu wilayani Geita hadi pale wamiliki watakapotimiza masharti waliyopewa pamoja na kurudisha dhahabu kilo 5.72 wanazodaiwa kutorosha Oktoba mwaka jana.

Mgodi huo ambao leseni ni yake ni ya Watanzania walioingia ubia na raia wa kigeni ulifungwa na wizara hiyo kwa kosa la kutorosha dhahabu lakini wamiliki wa leseni wanadai kosa hilo lilifanywa na wabia na sio wao.

Akizungumza baada ya kutembelea mgodi huo jana, Biteko alisema baadhi ya Watanzania siyo wema kwa wawekezaji na wanasababisha jina la nchi kuchafuliwa na wawekezaji kuogopa kuwekeza kutokana na ujanja ujanja unaofanywa na wazawa.

Amesema hata fungua mgodi huo hadi pale wamiliki watakaporudisha dhahabu iliyotoroshwa, kumaliza migogoro wa wao kwa wao kati ya wenye hisa na wakurugenzi.

Waziri huyo pia ameutaka mgodi huo kulipa madeni wanayodaiwa na watumishi zaidi ya Sh 284 milioni, kulipa tozo zote za Serikali wanazodaiwa pamoja na kulipa madeni ya na wanawaosambazia vifaa ‘Suppliers’.

“Hata nikiwafungulia Rais atanishangaa hawa waliiba dhahabu tumewaambia warudishe wameleta utapeli kuleta dhahabu feki, hawa wanadaiwa mamilioni hawajalipa niwafungulie vipi wana madeni na Serikali na suppliers hawajawalipa halafu mnaniambia niwafungulie acha waendelee na ujanja ujanja wao sitawafungulia hadi wakidhi vigezo,”amesema.

Biteko amedai wakurugenzi wa kampuni hiyo wanaishi maisha ya ujanja ujanja na kumtumia mtu anayetumia jina la Rais vibaya kwa kutembea ofisi mbalimbali kuchafua jina la wizara yake na kusema atasimamia sheria na kamwe hatarubuniwa na fedha kufanya jambo kinyume cha  utaratibu.

“Kwa mnayoyafanya hatuko tayari kuwafungulia na kwa makosa yenu naweza kuwafutia leseni endeleeni kuwachafua mnaowachafua kupita kila mlango ili muonekane wema lakini nawaambia mikono yangu ni misafi fedha mnazochanga tafuteni wa kumpa mimi nitasimamia sheria na taratibu,” alisema Biteko.

Fredy Masanja mmoja wa wakurugenzi wa mgodi huo, alisema dhahabu zilizoibiwa ziliibiwa na wabia wao ambao baada ya kukamatwa walilipa faini na kuondoka na kuacha mgodi huo ukiwa umefungwa.

Benson Matembi ambae ni msimamaizi wa mgodi huo aliiomba Serikali kuwahurumia watumishi waliopo na kufungua mgodi kwakuwa wanaoteseka zaidi ni watumishi na familia zao.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel aliishauri wizara ya madini kupitia mikataba ambayo wenye leseni wameingia ubia na wazawa kwakua mingi ipo kinyume cha sheria na inamnufaisha mwekezaji huku mwenye leseni akiwa hanufaiki.