Majaji, Ma-DC, DED walioteuliwa na Rais Magufuli hawa hapa

Muktasari:
Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa wakuu wa wilaya za Tarime na Mwanga sanjari na kuteua majaji 15 wa mahakama kuu na sita wa mahakama ya rufani
Pia amewateua wakurugenzi 10 ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi kwenye halmashauri za wilaya za mikoa mbalimbali nchini.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ametengua uteuzi wa wakuu wa wilaya za Tarime na Mwanga huku akiteua majaji 15 wa Mahakama Kuu na sita wa Mahakama ya Rufani.
Pia Rais Magufuli amewateua wakurugenzi 10 ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi kwenye halmashauri za mikoa mbalimbali nchini.
Taarifa ya Rais Magufuli iliyosomwa leo Jumapili Januari 27, 2019 kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi imeeleza kiongozi huyo ametengua uteuzi wa wakuu wa wilaya za Tarime, Glorious Luoga na Aaron Mbogho wa Mwanga.
“Nafasi ya Luoga imechukuliwa na Charles Kabeho aliyekuwa kiongozi wa mbio mwenge mwaka jana. Wakati nafasi ya Mbogho imechukuliwa na Thomas Apson,” amesema Balozi Kijazi.
Balozi Kijazi amewataja majaji wa Mahakama ya Rufani walioteuliwa ni Dk Rehema Sameji, Dk Mary Levira, Ignas Kitusi, Winnie Korosso, Lugano Mwandambo na Sahel Barke.
Majaji wa Mahakama Kuu ni Cyprian Mkeha, Dustan Ndunguru, Seif Kulita, Dk Mtemi Kilikamajenga, Zeferine Galeba, Dk Juliana Masabo, Mustafa Ismail, Upendo Madeha, Willbard Mashauri, Yohanne Masara, Dk Lilian Mongella, Fahamu Mtulya, John Kahyoza, Athuman Kirati na Suzan Mkapa.
Balozi Kijazi amewataja wakurugenzi wapya walioteuliwa kuwa na halmashauri zao kwenye mabano ni Isaya Mbenje (Pangani) Dk Fatuma Mganga (Hai) Regina Bieda (Tunduma) Jonas Malosa (Ulanga) Ali Juma Ali (Njombe) Misana Kangura (Nkasi) Diocres Rutema (Kibondo) Neto Ndilito (Mufindi) Elizabeth Gumbo (Itilima) Stephen Ndaki (Kishapu).
Majaji hao watapishwa Jumanne Januari 29, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam na Rais John Magufuli. Pia, Ma DC na Wakurugenzi watapaswa kuhudhuria shughuli hiyo.