Sakata la kampuni iliyofutiwa umiliki wa kitalu Arusha lachukua sura mpya

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla
Muktasari:
- Siku moja baada ya Serikali ya Tanzania kuifutia kampuni ya Green miles Safaris Ltd kitalu cha uwindaji wa kitalii cha Lake Natron East, mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe ameagiza kumarishwa ulinzi katika kitalu hicho.
Arusha. Siku moja baada ya Serikali ya Tanzania kuifutia kampuni ya Green miles Safaris Ltd kitalu cha uwindaji wa kitalii cha Lake Natron East, mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe ameagiza kumarishwa ulinzi katika kitalu hicho.
Jeshi la Polisi, madiwani na makatibu tarafa wa Longido, Kitumbeine na Engarinaibor ndio waliopewa jukumu la kuimarisha ulinzi huo ili kuzuia mali za mwekezaji hadi pale atakapolipa deni la Sh336 milioni analodaiwa na vijiji 23.
“Nawaagiza polisi wilaya ya Longido kuhakikisha wanaweka ulinzi wa kutosha wa mali zote zilizopo pale ili zisichukuliwe hadi tuhakikishe ameingiza fedha kwenye akaunti za vijiji. Vinginevyo tutavitaifisha vitu vyote na kwenda mahakamani ili vipigwe mnada,” amesema Mwaisumbe.
Jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla alitangaza kufuta kitalu hicho, na muda mfupi baadaye mkurugenzi wa kampuni hiyo, Awadh Abdallah alisema kitalu hicho hakijafutwa kama ilivyoelezwa na waziri huyo.
Leo Kigwangalla amelionyesha Mwananchi barua yake kwenda kwa meneja wa kampuni hiyo ya Agosti 7, 2019 yenye kumbukumbu namba CBA.177/389/01/281, akimueleza kuwa amefuta umiliki wa kitalu hicho.
Katika maelezo yake ya leo, Mwaisumbe amesema haiwezekani mwekezaji aje katika maeneo hayo ya wananchi na apewe masharti ya kufuata ikiwemo kuchangia kiasi cha fedha zinazopatikana na kupeleka kwenye vijiji, lakini hatekelezi jambo hilo.
Amebainisha kuwa alifika katika kijiji hicho mwaka 2013 na tangu wakati huo amekuwa hatoi ushirikiano kwa viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwemo wananchi.
Mkazi wa kata ya Mundarara wilayani Longido na mbunge wa zamani wa Longido, Lekule Laizer aepongeza hatua hiyo ya Serikali kwa maelezo kuwa wamekuwa wakisumbuliwa na mwekezaji huyo.
“Sijawahi kusikia mwindaji anapiga marufuku mifugo kuingia katika eneo la uwindaji wakati eneo hilo ndio ameweka kambi. Anawazuia wananchi kulisha mifugo yao wakati yeye ndio kawaingilia na bado amekataa kuwasaidia wananchi wanaozunguka eneo hilo,” amesema.
Diwani wa Mundurara, Alais Mushao naye alipongeza uamuzi huo kauli ambayo iliungwa mkono na wananchi wengine akiwemo Millya Kiloriti.