Wasichana wapewe elimu ya kuwashinda wakware

Licha ya kupigana kwa muda mrefu bado vita ya mimba na ndoa za utotoni haijawahi kumalizika.
Pamoja na kuwepo kwa sheria kali dhidi ya wanaotiwa hatiani kwa kosa la kumpa ujauzito mwanafunzi, wimbo huo kila siku unapata kiitikio kipya.
Kila kukicha taarifa za wasichana kupoteza masomo yao kwa sababu ya mimba zinaendelea kuripotiwa kwenye vyombo vya habari na zipo zisizojulikana.
Wakati vita hiyo ikidumu, Serikali na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za watoto, binadamu na usawa wa kijinsia yanaendelea kupaza sauti kupinga tatizo hilo.
Hata hivyo, wasichana wanaendelea kupoteza masomo kwa sababu hiyo. Nadhani ili kupambana na vita hiyo ni lazima kuangalia sababu zinazofanya wasichana washike mimba wakati wakiwa shuleni na nini kifanyike kumaliza sababu hizo?
Ukweli ni kwamba wanafunzi wa kike nchini wanaishi katika dunia mbili tofauti.
Dunia ya kwanza ni ya wale waliozaliwa na kusoma mijini wakikutana na changamoto zilizo tofauti na walio katika dunia ya vijijini.
Kwa mfano; mwanafunzi wa kike anayeishi mjini akiamka asubuhi hupanda daladala, pikipiki na wengine wanatembea ili wafike shuleni. Ikiwa atapanda daladala njiani atakutana na usumbufu wa kondakta, dereva ambao watataka kumpa lifti mpaka kituo atakachoshuka. Lifti za madereva bodaboda au daladala ndizo huanzisha mahusiano ya kimapenzi ambayo matokeo yake ni kuacha masomo kwa mimba. Ikiwa mwanafunzi huyo atakataa lifti, basi awe tayari kukaa kituo cha daladala kwa muda mrefu wakati mwingine inaweza kufika saa mbili usiku ndio anafika nyumbani kwao.
Huyu wa kijijini kwa sababu ya umbali na ukosefu wa nauli, wazazi watampangia chumba. Fedha ya matumizi atakayopewa huenda isimalize muhula, hivyo kila mwezi atatakiwa ama kwenda kuomba au kusubiri aletewe nyingine. Akiishiwa itabidi aende dukani kwa Masawe akakope na mwishowe huyu muuza duka ataamua kuanzisha uhusiano wa kimapenzi kwa sababu mwanafunzi huyo wa kike atakosa fedha ya kulipa.
Mara kodi ya nyumba inaisha wakati huo wazazi hawana habari mwishowe baba mwenye nyumba atamshaiwishi binti huyu mdogo kuingia nae katika uhusiano wa kimapenzi ili asilipe kodi.
Ukweli ni kwamba watoto wetu wa kike hawana ulinzi. Hata kama sheria inasema yeyote atakayempa mwanafunzi mimba atafungwa jela miaka 30 bado mzigo mzito wa malezi utamuangukia mtoto aliyeacha shule kwa sababu hiyo.
Ninachomaanisha hapa ni kwamba, ili kupambana na tatizo hili la mimba msichana lazima afundishwe wazi anajitoaje mwanaume anapomzonga. Ingewezekana somo hili lingeingia hata kwenye mtaala kuanzia darasa la tano. Katika makuzi yake afundishwe mbinu zitakazomsaidia kuwakwepa wanaume wakware wasio na staha.
Wasichana wengi hawana stadi za maisha na hawajui wanapokutana na tatizo kubwa kiuchumi wakimbilie wapi. Wakati mwingine wanashawishiwa na kudanganywa kwa zawadi ndogondogo ambazo mwisho wake ni mimba, kukataliwa na kupoteza masomo.
Kama wasichana hawa watafundishwa kuhusu dalili za mwanaume kutaka kuwashawishi waingie kwenye uhusiano na namna ya kujitoa kwa yule ambaye tayari ameanza kufanya ushawishi tatizo la mimba litapungua.
Kule wanako lazimishwa kuolewa wakiwa na umri mdogo lazima wapewe mbinu zitakazowasaidia kutoa taarifa wanapobaini dalili za kukatishwa masomo kwa sababu ya ndoa.