Mfumo mpya tiba kwa mtandao waja kurahisisha matibabu EAC

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akiwasha mwenge kama ishara ya ufunguzi wa kongamano la 7 la Afya na Sayansi la Afrika Mashariki lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais

Dar es Salaam. Mfumo mpya wa utoaji huduma za afya kwa njia ya mtandao unatarajiwa kumpunguzia gharama mwananchi na kuboresha matibabu ya kibingwa katika nchi za Afrika Mashariki (EAC).

Kulingana na mfumo huo, wananchi watanufaika kwa sababu hawatalazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za tiba kwa kuwa madaktari watakuwa na uwezo wa kuwasiliana na kusaidiana ili kutoa tiba.

Akizindua mfumo huo jijini hapa jana, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema mfumo huo utawezesha na kuongeza ufanisi wa uchunguzi, utoaji wa tiba na dawa kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali.

Alisema mfumo huo utapunguza gharama za wagonjwa na wanaowahudumia kusafiri kuwafuata madaktari kwa sababu kila kitu kitafanyika kwa njia hiyo.

Samia aliwaambia hayo mawaziri wa afya kutoka nchi za Afrika Mashariki waliojadili huduma hiyo kwa ajili ya kufanikisha malengo ya Umoja wa Mataifa.

Pia, alisema mfumo huo utarahisisha matibabu ya kibingwa na ushirikiano wa pamoja kati ya madaktari bingwa wa eneo hilo.

Samia alisema nchi za Afrika Mashariki zikijikita kutoa huduma kwa ushirikiano wa pamoja, itakuwa ni njia sahihi kufikia malengo ya milenia na huduma za afya kwa wote. “Tunapaswa kufikia malengo tuliyojiwekea kama bara la Afrika na nchi za Afrika Mashariki,” alisema.

Waziri wa Afya na Mapambano dhidi ya VVU kutoka Burundi, Dk Thaddee Ndikumana alisema, “wananchi wa Burundi wataweza kupatiwa matibabu na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwa nchini kwao bila kuja Dar es Salaam.”

“Hiyo ni muhimu, tutakuwa tunabadilishana uzoefu, raia wa Burundi walikuwa wanakuja kila siku, sasa safari zitapungua, watabaki Bunjumbura na huduma watapata.”

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema kulingana na mfumo huo daktari atakuwa na uwezo wa kuwasiliana na wenzake wa nchi nzima na wakaona tatizo linalomsumbua mgonjwa.

“Nchini Tanzania miezi mitatu iliyopita madaktari walianzisha mfumo wa mawasiliano kupitia dijitali ambao unawawezesha madaktari bingwa kuwasiliana moja kwa moja na madaktari waliopo pembezoni, na umeweza kuokoa maisha ya kinamama sita ambao walikuwa wanajifungua,” alisema Ummy.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr), Profesa Yunus Mgaya alisema mfumo huo utapunguza gharama za utoaji wa huduma za afya na kuongeza ufanisi wa wahudumu wa afya katika utekelezaji wa majukumu yao.