Leseni za madini kufutwa

Naibu waziri wa Madini, Staslaus Nyongo

Muktasari:

Naibu waziri wa Madini, Staslaus Nyongo wizara yake imeanza kufuatilia uhalali wa leseni 86 za uchimbaji madini ndani ya eneo la hifadhi ya jamii ya wanyamapori (WMA) ya Makao wilayani Meatu ili kuzifuta.

Dar es Salaam. Wizara ya Madini, imeanza kufuatilia uhalali wa leseni 86 za uchimbaji madini ndani ya eneo la hifadhi ya jamii ya wanyamapori (WMA) ya Makao wilayani Meatu ili kuzifuta.

Leseni hizo zilitolewa tangu mwaka 2016 kwa wachimbaji wadogo, kuchimba dhahabu na madini ya shaba eneo hilo linalopakana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Akizungumza na gazeti hili jana, naibu waziri wa Madini, Staslaus Nyongo alisema kawaida leseni za kuchimba dhahabu au shaba hazitolewi katika maeneo ya hifadhi.

“Wizara huwa tunatoa leseni za uchimbaji kama eneo linakidhi vigezo, lakini kama ni hifadhi hairuhusiwi kuchimba na tutafuta hizo leseni,” alisema.

Hata hivyo, tangu kutolewa kwa leseni hizo na kufanyika uchunguzi wa athari za uharibifu wa mazingira (EIA), Wizara ya Maliasili na Utalii ilipinga kupitia aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Profesa Jumanne Maghembe.

Naye ofisa wanyamapori wa wilaya ya Meatu, Revocatus Meney alisema uchimbaji madini utakuwa na athari kubwa kwa wanyamapori na mazingira.

“Waliopewa leseni wamekuja mara kadhaa eneo hili na Mto Gururu kuchukua sampuli ya miamba, lakini tayari maofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (Nemc) wamefika kuchunguza eneo hili,” alisema Meney.

Alisema anaamini wizara ya Madini itafanya uchunguzi kubaini uhalali wa leseni hizo.