Chuo cha Utalii kufundisha shahada ya ukarimu na utalii

Mtendaji mkuu wa NCT, Dk Shogo Sedoyeka

Muktasari:

Katika jitihada za kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea vivutio vya utalii Tanzania pamoja na kuimarisha huduma za hoteli zilizopo, Chuo cha Taifa cha Utalii kitaanza kutoa shahada ya utalii na ukarimu kuwapa fursa wahitimu wake kushika nafasi za juu kwenye hoteli za kitalii nchini.

Dar es Salaam. Ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaoongoza hoteli za kitalii nchini, Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kitaanza kufundisha shahada ya ukarimu na utalii kuanzia Septemba mwakani.

Mtendaji mkuu wa NCT, Dk Shogo Sedoyeka amebainisha hilo jana, Oktoba 14 alipokuwa anamueleza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga kuhusu mikakati iliyopo. Hasunga alifanya ziara kampasi ya chuo hicho Temeke na Bustanini.

Kwa mara ya kwanza, Dk Sedoyeka amesema chuo hicho kitaanza kuzalisha wataalamu wanaokidhi mahitaji ya soko katika sekta ya utalii hasa mameneja wa hoteli zilizopo na zitakazojengwa na idara za utalii.

"Tunaendelea kukamilisha baadhi ya utaratibu tulioelekezwa ili mwakani tuanze kutoa shahada ya kwanza," alisema Dk Sedoyeka.

Kwa upande wake, Hasunga alisema hatua hiyo ni muhimu kwa ustawi wa sekta ya utalii kwani kwa muda mrefu wageni wamekuwa wakishika nafasi za juu katika fani ya ukarimu kwa madai kuwa Watanzania hawana  sifa.

Waziri huyo amesema anaamini chuo hicho kitazalisha wahitimu wenye uwezo wa kuongeza mchango wa hoteli za kitalii, kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea vivutio vilivyopo nchini hivyo kukuza mapato na uchumi kwa ujumla.

Kufanikisha dhamira hiyo, Hasunga amewaagiza wakufunzi: “Fanyeni utafiti na kuandika machapisho ya kitaaluma kuhusu utalii na ukarimu yatakayosaidia kuwaandaa wanafunzi wanaohitajika sokoni.”

Aidha, waziri huyo ametoa miezi mitatu mpaka Januari chuo hicho kianze kuchapisha jarida la kitaalamu la masuala ya utalii likijielekeza zaidi kwenye masuala ya hoteli.

Licha ya kuwa kati ya nchi zenye vivutio vingi duniani, Tanzania inapokea chini ya watalii milioni 1.5 huku kukosekana kwa matangazo kwenye masoko makubwa na wataalamu wa sekta hiyo zikitajwa kuwa miongoni mwa changamoto zilizopo.