Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MAONI: Wizara ielimishe wimbo, bendera ya Taifa

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imevielekeza vyuo vya ualimu, vyuo vikuu na taasisi nyingine zilizo chini yake kutumia kwa usahihi alama kuu za Taifa.

Barua iliyoandikwa kwa vyuo hivyo inaeleza kuwa alama hizo, ambazo ni Wimbo wa Taifa na Bendera ya Taifa zimekuwa zikitumika isivyo sahihi na hivyo kutaka hali hiyo irekebishwe.

Barua hiyo inaeleza kuwa Wimbo wa Taifa inabidi uimbwe katika hafla maalumu na mafungu yote mawili, wakati ikikosoa matumizi ya rangi ya njano katika bendera hiyo kuwa si sahihi. Inasema rangi ya dhahabu ndiyo sahihi.

Kitu hicho ama kilieleweka vibaya au hakikuwa kikieleweka na kusababisha watengenezaji au washonaji wengi wa bendera hiyo kutumia rangi ya njano.

Uamuzi wa wizara kukumbusha matumizi ya alama hizo ni muhimu, lakini kitendo cha watendaji wake kutotaka kutoa ufafanuzi katika suala hilo muhimu kinatia wasiwasi.

Kila mara waandishi wa habari walipoomba ufafanuzi kuhusu barua hiyo, maofisa na watendaji wa wizara walijibu kwa kifupi kuwa barua iliyosambaa mitandaoni ni yao, lakini wakasema haiwahusu waandishi bali vyuo vilivyoandikiwa.

Watendaji na maofisa hawa wamesahau kuwa Bendera na Wimbo wa Taifa unawahusu Watanzania wote ambao kutokana na ukereketwa wa uzalendo wao, wana hamu ya kuuimba au kutumia rangi za bendera yetu kuonyesha wanavyojivunia utaifa wao.

Wimbo wa Taifa na Bendera ya Taifa hazitumiwi na vyuo pekee, bali kila Mtanzania kulingana na jambo analolifanya au mahali alipo. Wanamichezo wanatumia alama hizo wanapokuwa katika mashindano ya kimataifa na wanaona ufahari kubeba bendera ya nchi yao pale wanaposhinda.

Hali kadhalika wanamuziki au maofisa wengine wanapochanganyika na watu wa mataifa mengine.

Washonaji wa nguo pia wangependa kutambulisha mavazi ya Kitanzania kwa kuweka Bendera ya Taifa, hali kadhalika waandaaji wa mashindano, maonyesho au matamasha makubwa wangependa rangi hizo zipambe shughuli zao au wimbo huo uimbwe kuzindua matamasha yao.

Pamoja na ukweli kwamba, vyuo au taasisi nyingine za elimu zinatoa wasomi watakaokuja kufundisha watoto wetu umuhimu wa alama hizo, bado kizazi kilichopo kinahitaji kujua matumizi sahihi ya Wimbo na Bendera ya Taifa ili kisije kujikuta katika mikono ya sheria kwa jambo ambalo linaepukika.

Wizara ya Elimu ina jukumu la kuelimisha wananchi wote kuhusu nembo hizo muhimu ili wananchi wajue wanatakiwa kufanya nini kila wanapoona haja ya kutumia Wimbo wa Taifa au Bendera ya Taifa. Suala hilo halipaswi kuwa siri ya vyuo hivyo tu, hata kama barua hiyo ilielekezwa huko pekee.

Wakati huu ambao Rais John Magufuli anahimiza wananchi kuwa wazalendo, vitu vinavyojenga, kutangaza au kuonyesha uzalendo kama alama hizo za Taifa, ni lazima vieleweke vizuri kwa kila Mtanzania.

Wakati huu ambao vijana wanaona ufahari kuvaa fulana zenye bendera za Marekani, Uingereza au Jamaica, hautakiwi uwe na mazingira yasiyoeleweka kuhusu bendera yao, bali elimu na uhamasishaji wa kutosha kubadili fikra hizo.