Mtaalamu aeleza matumizi ya viazi lishe

Viazi vitamu vyenye rangi ya karoti kwa ndani ambavyo vina vitamin A kwa wingi vinaitwa viazi lishe.
Viazi lishe vina manufaa kwa jamii hasa kwa watoto na kinamama walio katika umri wa kuzaa ambao wako katika hatari ya kupata upungufu wa virutubisho vya vitamin A.
Mtaalamu wa Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Cypriana Cyprian anasema vitamin A inayopatikina katika viazi lishe husaidia kuimarisha kinga ya mwili na kuepuka uoni hafifu.
“Wanga uliopo katika viazi husaidia kuupa mwili nguvu na nyuzinyuzi zilizopo katika viazi hivi, hu-rahisisha umeng’enyaji wa chakula tumbo-ni,”anasema Cyprian.
Anafafanua kuwa viazi lishe vina aina nyingi za vit-amin B, C na K, ambazo ni muhimu kwa ukuaji na afya nzuri ya mwili.
Pia, anabainisha matumizi ya viazi lishe ukiachilia mbali kuchemsha na kukaanga kama ilivyo kwenye aina nyingine ya viazi, vinafaa kutengenezwa chipsi, juisi, kripsi na unga wa lishe kwa watoto wadogo.
“Unga wa viazi lishe unaweza kuchanganywa na unga wa ngano ili kutengeneza mikate, chapati, maandazi na aina nyingine za vitafunwa,” anasema Cyprian.
Mtaalamu huyo wa masuala ya lishe, anasema hapa nchini kuna aina nyingi za viazi lishe ambazo zimethibitishwa na watalaamu; kati ya hivyo ni mataya, kiegeya, ejumula na kakamega.
Cyprian anasema kwa sasa watafiti wako mbioni kutoa aina nyingine ya viazi lishe, katika kituo cha utafiti cha Kibaha.
Hata hivyo, daktari bingwa wa macho kutoka Hospitali ya Duke, Dk Jill Koury anasema upungufu wa Vitamini A unasababisha sehemu ya jicho inayopokea mwanga kuharibika na kusababisha uoni hafifu.
Makala haya yameandikwa na mwandishi wa gazeti hili, Hadija Jumanne.