Timu ya Taifa ya Tembo Warriors kutua bungeni

Muktasari:

  • Mashindano ya soka ya watu wenye ulemavu yatafanyika Jijini Dar es Salaam yatashirikisha nchi tano (5) Tanzania Bara ikiwa mwenyeji

Dodoma.Timu ya mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu (Tembo Warriors) itakuwa bungeni Alhamisi Mei 23, 2019, wachezaji watapata nafasi ya kuwaambia wabunge juu ya mikakati yao.

Mwenyekiti wa wabunge wenye ulemavu Riziki Lulida amesema kikosi cha wachezaji 15 kitakuja bungeni wako tayari kuonyesha vipaji vyao.

Lulida amesema timu hiyo iko katika kipindi cha mwisho kuelekea kambi kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya mpira kwa wenye ulemavu Afrika Mashariki.

Mashindano hayo yatakayofanyika Jijini Dar es Salaam yatashirikisha nchi tano (5) Tanzania Bara ikiwa mwenyeji.

Mwenyekiti huyo ameomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwatia moyo wachezaji hao waliopania kubakisha kombe kutokana na maandalizi yao ili kulinda heshima ya nchi.

Balozi wa watu wenye ulemavu, Mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto amesema timu hiyo bado inakabiliwa na ukata pamoja na vifaa vyao kuzuiliwa bandari kwa kukosa Sh7 milioni.

Mwamoto amewataka wadau na wabunge kujitokeza kuisaidia timu hiyo kwani baada ya timu zingine kushindwa, Tembo inategemea kubakiza kombe nchini.