Rais atishia kuzuia wachezaji wa Bayern kuchezea timu ya taifa

Muktasari:

Kipa wa Bayern Munich, Manuel Neuer na wa Barcelona, Marc-Andre Ter Stegen wameingia kwenye mzozo wa maneno kugombea nafasi katika kikosi cha taifa.

Rais wa Bayern Munich, Uli Hoeness ametishia kuwazuia wachezaji wa klabu hiyo kuchezea timu ya taifa kama Manuel Neuer atapoteza nafasi yake ya kuwa kipa wa kwanza wa Ujerumani, gazeti la Sport Bild limeripoti leo Jumatano.
Kipa wa Barcelona, Marc-Andre Ter Stegen, 27, kwa sasa ni kipa wa pili wa Neuer na ameeleza kutofurahishwa na kuwekwa benchi katika timu ya taifa na kipa huyo mzoefu wa Bayern Munich.
wachezaji hao wawili wametupiana maneno na wiki iliyopita Ter Stegen alimtuhumu Neuer kusema "maneno ambayo si sahihi".
Hoeness, hata hivyo, amezungumza kwa niaba ya Neuer na kumkosoa kocha wa Ujerumani, Joachim Low na Shirikisho la Soka la Ujerumani kwa kutowalinda wachezaji nyota wa Bayern kwa kupaza sauti.
"Hatutalikubali hilo kwamba kutakuwa na mabadiliko," gazeti hilo la michezo la kila siku lilimkariri Hoeness.
"Kabla hilo halijatokea tutawazuia wachezaji wetu wote kujiunga na timu ya taifa."
Pamoja na Neuer, Bayern imechangia wachezaji muhimu kwenye kikosi cha taifa na hivyo kitendo chochote cha kuwazuia kitamfanya Low akose huduma ya beki Niklas Suele, viungo Joshua Kimmich na Leon Goretzka pamoja na mshambuliaji Serge Gnabry.
Low aliahidi kumpa Ter Stegen muda zaidi wa kucheza mwaka 2019 lakini hadi sasa amecheza mechi moja tu, akicheza kwa dakika 45 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Serbia mwezi Machi.
Chini ya sheria za FIFA, Bayern inaweza kukabiliwa na adhabu ya kuanzia kutozwa faini hadi kuondolewa kutoka katika mashindano ya chama hicho cha soka barani Ulaya kwa kuzuia wachezaji wake kuchezea timu ya taifa.