VIDEO: Kilichotokea baada ya Kagere, Shiboub kutua Kanda ya Ziwa

Muktasari:

Hadi sasa Kagere anaongoza kwa ufungaji mabao akiwa na matano baada ya mechi tatu walizocheza Simba na kuifanya timu yake kuongoza Ligi Kuu kwa alama tisa.

STRAIKA wa Simba, Meddie Kagere ameendelea kuwakuna mashabiki wa timu hiyo baada leo Ijumaa jina lake kutajwa mara dufu wakati timu hiyo ikiwasili jijini hapa ikitokea mkoani Kagera.
Simba jana Alhamisi ilicheza mechi yao ya tatu ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar na kupata ushindi wa bao 3-0 huku mabao mawili yakifungwa na Kagere.
Kagere anasifika kwa kasi yake uwanjani na ufungaji mabao hadi sasa amefunga mabao matano katika mechi hizo tatu walizocheza.
Mashabiki waliojitokeza kukipokea kikosi hicho Uwanja wa Ndege wa Mwanza, jina la Kagere walilitaja zaidi pamoja na la Shiboub Sharaf na kuwafanya wananchi waliokuwa uwanjani hapo kubaki na vicheko.
"Kagere, Kagere, Kagere Kagereeee...Shiboub" zilisikika sauti za mashabiki wakati Simba ikiwasili.
Wekundu hao watakuwa Mwanza leo Ijumaa wakijifua jioni na kesho Jumamosi asubuhi kisha mchana kuelekea mkoani Mara kuwakabili Biashara United ambao watacheza nao keshokutwa Jumapili uwanja wa Kumbukumbu ya Karume