Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAGUZI UPINZANI 2015: Dk Emmanuel Makaidi, Mwenyekiti NLD

WASIFU
Umri: Miaka 74
Elimu: Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Howard, Marekani
Kazi: Mwenyekiti wa Chama cha NLD

Muktasari:

  • Dk Makaidi alijitosa katika mbio za ubunge kwa mara ya kwanza mwaka 2010 katika Jimbo la Masasi, Mtwara akipambana na Mariam Kasembe wa CCM (aliyeibuka mshindi wa jumla kwa asilimia 63.7) na Clara Mwatuka wa CUF (aliyepata asilimia 15.2). Katika uchaguzi huo Dk Makaidi alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 5,384 sawa na asilimia 11.7 ya kura zote zilizopigwa.

Historia yake

Dk Emmanuel Makaidi ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NLD na ni mhandisi aliyebobea. Alizaliwa Aprili 10, 1941 huko wilayani Masasi mkoani Mtwara. Baba yake mzazi alikuwa ni katekista wa Kanisa la Anglikana.

Alianza elimu katika Shule ya Msingi Namalenga wilayani Masasi kati ya mwaka 1948 – 1952, mwaka 1953 – 1954 alisoma katika Shule ya Kati (Middle school) iitwayo Luatala hukohuko Masasi. Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari ya Chuo cha Mtakatifu Joseph na kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne kati ya mwaka 1953 hadi 1956.

Makaidi alisoma darasa la 13 na 14 (kidato cha tano na sita) katika Shule ya Sekondari Luhule, Uganda kati ya mwaka 1957 – 1958. Alipelekwa Uganda si kwa sababu ya kipato cha baba yake, la hasha, alisaidiwa na Askofu wa Anglikana baada ya kuona anafaulu mitihani yake kwa alama za juu sana.

Makaidi aliendelea kufadhiliwa na askofu huyo ambaye alimuunganisha na mashirika mengine na kumtafutia chuo Afrika ya Kusini. Akapelekwa Chuo Kikuu cha Witwatersrand na kuhitimu Shahada ya Uendeshaji na Usimamizi kati ya mwaka 1958 – 1960.

Baada ya kuhitimu vizuri pale Witts, aliendelea kupata ufadhili wa masomo ya shahada ya uzamili, mara hii alielekea Marekani na kusoma masuala ya Menejimenti na Utawala kwa ngazi ya uzamili kati ya mwaka 1960 – 1962. Alisoma pia katika Chuo Kikuu cha Howard kilichoko jijini Washington, Marekani.

Baada ya kurejea nchini akiwa mhitimu wa M.A, Makaidi alianza kazi serikalini mwaka 1966 hadi mwaka 1973 akiwa mchambuzi kazi mkuu, katika kitengo cha Utumishi.

Kati ya mwaka 1974 na 1975 (miaka miwili). Alirudi tena Marekani na kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Howard akipata kuwa karibu na mmoja wa maprofesa nguli duniani, Wamba Dia Wamba. Makaidi ameniambia kuwa hata tabia ya kuandika vitabu na kutunga mambo ya ubunifu, alifundishwa na profesa huyu mahiri.

Aliporejea nchini kwa mara ya pili mwaka 1976 aliendelea na kazi yake pale Utumishi hadi mwaka 1985 alipopewa kazi nyingine kubwa zaidi, akawa Mkurugenzi wa Miundo na Mishahara kwenye kamati iliyokuwa inashughulikia mashirika ya umma nchini.

Wakati anaendelea na kazi utumishi, alipata fursa nyingine ya kusomea stashahada ya Kuchakata Taarifa za Kielektoniki katika Chuo Kikuu cha Trinity, Ireland. Alikwenda huko na kuhitimu mwaka huohuo 1977.

Kabla hajafanya kazi katika kamati maalum ya kusimamia mashirika ya umma akapandishwa cheo na kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Ustawi wa Jamii na mwaka huohuo 1985 akafukuzwa kazi.

Kisa cha Makaidi kufukuzwa kazi serikalini, tena akiwa na wadhifa huo ilikuwa ni kwa sababu ya kuandika kitabu cha Kiingereza chenye jina “mwanasiasa mwenye roho ya shetani”. Serikali ikamzonga vilivyo, ikamtuhumu kuwa kitabu kile kinamtukana Mwalimu Julius Nyerere. Mwisho wa siku “kazi ikaota mbawa”.

Bahati nzuri, mwaka huohuo 1985 akaajiriwa na Shirika la Finwork Directory kuwa Mkurugenzi Mtendaji, kazi aliyoifanya hadi mwaka 1991.

Kuanzia mwaka 1992 hadi hivi leo, Dk Makaidi hajajishughulisha tena na kazi za serikalini wala mashirika binafsi. Amejiajiri akiwa na kampuni kadhaa zilizoajiri Watanzania wa vipato vya kawaida, lakini pia ameendelea kutoa ushauri wa kitaalamu kwa kampuni za ndani na nje ya nchi huku akiongoza chama cha NLD akiwa Mwenyekiti.

Dk Makaidi ni mwandishi mzuri wa vitabu, ameshaandika zaidi ya 10. Amemuoa Modesta Ponela na wana watoto wanane.

Mbio za ubunge

Dk Makaidi alijitosa katika mbio za ubunge kwa mara ya kwanza mwaka 2010 katika Jimbo la Masasi, Mtwara akipambana na Mariam Kasembe wa CCM (aliyeibuka mshindi wa jumla kwa asilimia 63.7) na Clara Mwatuka wa CUF (aliyepata asilimia 15.2). Katika uchaguzi huo Dk Makaidi alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 5,384 sawa na asilimia 11.7 ya kura zote zilizopigwa.

Januari 2014, Dk Makaidi alikuwa mmoja wa Watanzania walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ambalo liliendeleza mchakato wa kikatiba, ulioanzishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Mbio za urais

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Dk Makaidi alipitishwa na chama chake, NLD, kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni mmoja wa wagombea waliofika katika maeneo kadhaa ya nchi kuomba kura pamoja na kuwa chama chake hakikuwa na nguvu kubwa ya kisiasa na hata uchumi. Kwenye uchaguzi ule ambao mshindi alikuwa Kikwete, Dk Makaidi alipata asilimia 0.19 ya kura zote zilizopigwa na kushika nafasi ya saba kati ya wagombea 10 waliokuwa wanashindana.

Katika mbio za urais za mwaka huu, NLD tayari kimeshampitisha tena kuwa mgombea wake na kinasubiri tu ridhaa ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuona kama ndiye atakayepewa nafasi hiyo au la.

Makubaliano ya ndani ya Ukawa ya namna ya kumpata mgombea urais wake, hayajawekwa wazi hadi hivi sasa japokuwa vyama vinavyounda umoja huo vinaweza kukiachia chama kimoja kiteue mgombea urais au vinaweza kushindanisha wagombea wa vyama vyote na kumchukua mmoja wa jumla ambaye anaweza tena kukabidhiwa kwa chama chake cha awali ili agombee.

Sheria za Tanzania kwa sasa haziruhusu vyama kuungana kabla ya uchaguzi na jambo hilo lina maana kuwa mgombea mmoja atakayeteuliwa na umoja huo, atagombea kupitia katika chama chake kilichosajiliwa na viongozi wa vyama vingine watakuwa na jukumu la kuhamasisha wanachama wao wampigie kura mgombea wa chama hicho kwenye uchaguzi.

Nguvu yake

Jambo la kwanza linalombeba Dk Makaidi ni elimu. Yeye ni mmoja wa Watanzania wachache waliosoma na kufikia ngazi ya shahada ya uzamivu. Amenijulisha kwamba amesoma kwa shida tangu alipokuwa kijana mdogo na hata alipokuwa kazini, lakini aliweka juhudi kubwa. Elimu ya ngazi aliyonayo ni bora kwa mtu anayetaka kuongoza nchi.

Lakini jambo la pili, yeye ni kati ya wajasiriamali waliothubutu kuanzisha shughuli za kujiingizia kipato na kuajiri Watanzania wengine huku akiendelea na kazi ya kuwatetea wananchi kupitia siasa. Dhana ya ujasiriamali inakua duniani hivi sasa na mtu yeyote mwenye uzoefu mkubwa na sekta ya soko huria, anafahamu matatizo ya wananchi wa chini kwa karibu na sifa hii ina umuhimu wake katika kuongoza Taifa lililojaa walalahoi na watu wa chini.

Tatu, Dk Makaidi hajawahi kuwa mwanachama wa Tanu wala CCM. Ameniambia kuwa tangu zamani alikuwa anakiona chama kinachoongoza dola kwa jicho baya, hakuamini kama siku moja kingelikuja kulibadilisha Taifa hili na kwa hivyo aliweka msimamo wa kutojiunga nacho. Anasema yeye ni mmoja wa Watanzania wachache ambao wanaweza kujipiga kifuani hadharani na kutamba kuwa kwa umri wake hakuwahi kuwa mwanachama wa CCM.

Lakini sifa na nguvu ya nne ya Dk Makaidi ni msimamo. Kiongozi huyu ni mmoja wa wanasiasa wanaotoka kwenye vyama vinavyokua au kujiimarisha, akiwa na msimamo thabiti katika masuala ya msingi. Si mtu wa kuyumbishwa na fedha au ukuu, si mtu wa kutumika au kutumiwa, anasimamia ajenda anazozijua na kuziamini.

Katika Bunge Maalumu la Katiba, Dk Makaidi ni mmoja wa viongozi waliounda Ukawa walioamua kuondoka. Hakujali kupoteza mamilioni ya fedha za posho, alishikilia msimamo na kuzitosa fedha. Alisimamia misingi ya kusaka katiba bora aliyokuwa anaiamini na tokea hapo amekuwa moja ya mihimili mikubwa ya Ukawa.

Ni wanasiasa au viongozi wangapi wa vyama visivyo na wabunge kama yeye walioweza kuondoka Dodoma na kuacha posho kwa ajili ya kupigania masilahi mapana ya Taifa? Ndiyo maana Makaidi anakuwa mmoja wa Watanzania ambao wana vigezo na sifa za kuwa kiongozi mkubwa zaidi.

Udhaifu wake

Moja ya jambo ninalolitizama kama udhaifu wa Dk Makaidi ni kutoweza kukikuza chama chake kupata wabunge. NLD ni moja kati ya vyama visivyo na wabunge na yeye ndiye mwenyekiti wake. Pamoja na ile dhana kuwa vyama vyenye wabunge vina nguvu kubwa ya rasilimali fedha na watu nyakati za uchaguzi, hiyo haiondoi ukweli kuwa hata vyenyewe kuna wakati havikuwahi kuwa na wabunge lakini vilipambana hadi kuanza kupata wabunge. Kutofanikiwa kukikuza chama chake kuwa katika ngazi ya juu ya ushindani wa kisiasa, kunaweza kutafsiriwa kama “kushindwa kupenya” vizingiti vya siasa za vyama kabla hajakabidhiwa majukumu makubwa ya nchi.

Lakini pili, naona kama Dk Makaidi ana udhaifu katika eneo la kutoa taarifa kwa umma na labda kupitia katika vyombo vya habari. Hivi karibuni alipohojiwa na juu ya hatua ya chama kimoja ambacho kinaunda Ukawa kuanza kura za maoni za ndani ilhali makubaliano ambayo hayajakamilika, Dk Makaidi alitoa kauli zinazoashiria namna ambavyo hakuwa anaridhishwa na hatua ile.

Kwa mtizamo wangu, yale ni masuala ambayo angepaswa kuzungumza na viongozi wenzake wa Ukawa au kuwasiliana na viongozi wa chama kile kilichoanza kura za maoni na kujua namna ya kuwasiliana na waandishi. Moja ya mambo ambayo mkuu yeyote wa nchi anapaswa kujifunza na kuyashikilia ni anatoa habari zipi, kwa nani, kwa nini na zitaleta madhara gani. Japokuwa hili ni jambo la mtu kujifunza zaidi, lakini kwa kiongozi ambaye anatajwa kuwa na sifa za kuwa rais, ni upungufu mkubwa.

Nini kimemfanya apitishwe NLD?

Moja ya mambo yaliyofanya NLD impitishe kuwa mgombea urais wake ambaye ataomba kibali cha Ukawa kupeperusha bendera ya umoja huo ni kwa sababu ni mwanasiasa maarufu kuliko mwingine yeyote ndani ya chama chake. Ningeshangaa kama NLD wangefikiria kumpeleka mwanachama mwingine ambaye hana uzoefu wa kisiasa au asiyefahamika kama ilivyo Dk Makaidi.

Lakini pili, nadhani amepitishwa kwa sababu ya uzoefu wake katika kufanya kazi serikalini. Amekuwa mtumishi wa Serikali kwa zaidi ya miongo mitatu. Huu ni muda mrefu katika shughuli za utumishi wa umma. Lakini pia amekuwa mfanyakazi wa ngazi ya juu katika sekta binafsi na hivyo anajua changamoto za ndani ya Serikali na katika sekta binafsi.

Tatu, naona amepitishwa kwa sababu yeye ni mmoja wa waasisi wa Ukawa. Isingekuwa jambo la busara kwa chama chake kumpitisha mgombea ambaye hafahamu vizuri misingi ya uanzishwaji wa umoja huo, malengo na dira yake kwani ingekuwa kazi rahisi kuangushwa na wagombea wengine wenye wasifu mkubwa kumshinda. Faida ya kufahamu Ukawa ni muhimu kwa ajili ya kulinda masilahi ya chama kinachokua kama NLD.

Nini kinaweza kumwangusha?

Mambo mawili makubwa yanaweza kumwangusha katika mchujo wa ndani ya Ukawa, maana ameshapita ule wa ndani ya chama chake.

Moja ni ikiwa umoja huo utaamua moja kwa moja kuwa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia umoja huo igombewe na moja ya chama kinachounda umoja huo na kisicho NLD, ‘automatically’ atakuwa amekosa fursa hiyo muhimu.

Lakini jambo la pili linaloweza kumwangusha kwenye mchujo ni ikiwa wagombea wa Ukawa watapambanishwa bila kuangaliwa wanatoka chama gani. Huenda jambo hili likamwangusha kwa sababu ndani ya Ukawa kuna viongozi wenye sifa nyingi zaidi, uzoefu mkubwa zaidi wa kitaifa na kimataifa na wakiwa miongoni mwa Watanzania mashuhuri kumpita.

Mwisho, jambo linaloweza kumkwamisha, ni ikiwa mgombea wa Ukawa atapaswa kutoka Zanzibar. Kwa sababu yeye ni Mtanzania mwenye asili ya Bara, hii ni sababu isiyo na majadiliano na inaweza pia kukiathiri chama chake kwa sababu hata huko Zanzibar nimeambiwa kina wanachama wa kawaida wasio na sifa kubwa kama za kwake.

Asipopitishwa (Mpango B)

Dk Makaidi atakuwa na mipango kama minne ikiwa hatapitishwa kugombea urais kupitia Ukawa:

Jambo la kwanza atakalofanya linaweza kuwa ni kugombea ubunge katika Jimbo la Masasi ambalo aligombea mwaka 2010. Dk Makaidi ni mwanasiasa mwenye uwezo mkubwa na tuliona uthubutu wake, uwezo wa kujenga hoja na kufanya utafiti kama alivyouonyesha katiba Bunge Maalumu la Katiba, naamini akiwa mbunge anaweza kuwa na mchango mkubwa zaidi kwa Taifa.

Lakini jambo la pili, kwa sababu kiongozi huyu ni mjasiriamali wa muda mrefu na mtu mwenye uzoefu na sekta ya umma na ile binafsi, anaweza kuendelea na ujasiriamali wa juu zaidi akiajiri vijana wa Kitanzania wengi zaidi kwa kuangalia mahitaji ya sekta ya umma na wananchi kwa ujumla na kuona namna wanavyoweza kupata huduma za ubunifu.

Jambo la tatu analoweza kufanya ni kutoa ushauri na kufundisha. Kwa sababu ana shahada ya uzamivu, natambua kuwa kuna vyuo vingi vipya vimeanzishwa hivi karibuni lakini vikiwa havina walimu wa kutosha. Kama anafikia vigezo, anaweza kuungana navyo na kuendelea kuwasaidia vijana kitaaluma. Lakini kwa kuunganisha, anaweza pia kuendelea na kazi za kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wajasiriamali wanaokua na wale wanaojifunza, bila kusahau kampuni za ndani na nje.

Hitimisho

Rais wa Afrika ya Kusini, Jacob Zuma hana hata shahada moja ya chuo kikuu na elimu yake haieleweki hadi leo, uzoefu wa kisiasa peke yake umemtosha kuongoza Taifa kubwa kabisa Afrika. Dk Makaidi ana uzoefu wa kisiasa ndani ya nchi na ni msomi, naamini anao uwezo mkubwa lakini itampasa azidi kujipanga hata akikosa tiketi ya urais kwa Ukawa.

Lakini pia, chama chake kimepata fursa muhimu ya kuwamo katika muungano wa vyama vya siasa vitatu vyenye wabunge na ambavyo unaweza kusema ndivyo vyenye nguvu hapa Tanzania, ukiachilia mbali CCM. Kuwamo kwenye muungano na vyama hivi ni fursa pekee kwake kisiasa, lakini pia kwa chama chake.

Ni matumaini yangu kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu, Dk Makaidi atakuwa mwanasiasa mwenye taswira ya juu zaidi, lakini pia chama chake walau kitakuwa na wawakilishi huku na kule.

Binafsi nampongeza kwa kuendelea kuwa mwana mabadiliko lakini zaidi ya yote kwa safari yake ya kisiasa ambayo naamini bado haijafika mwisho.

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii; ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa (B.A) katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (LLB) – Anapatikana kupitia +255787536759.
Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni yake binafsi.