|
Na Peter Edson
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikisema kuwa mazungumzo ya muafaka wa Zanzibar yanatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya Chama Cha Wananchi (CUF) kukubali kurudi kwenye meza ya mazungumzo, chama hicho kimesema hakina taarifa.
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa CUF, Ismail Jussa, aliliambia gazeti hili jana kuwa taarifa ya CCM kwamba CUF imekubali kurudi katika meza ya mazungumzo sio kweli kwasababu hawajawasiliana na CCM kuhusu jambo hilo.
Jusa alisema hawana taarifa zozote kuhusiana na kikao kama viongozi wa CCM walivyodai na kusisitiza kwamba mazungumzo hayo hayapo.
Jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Kapteni John Chiligati, aliwaambia waandishi wa habari kuwa baada ya vuta nikuvute iliyodumu kwa miezi saba sasa kuhusu mazungumzo hayo, CUF sasa imekubali kurudi mezani.
“Wenzetu wa CUF wamekubali kurudi kwenye meza ya mazungumzo, tunachokisubiri ni kupangwa kwa tarehe ya kuanza upya mazungumzo hayo itakayotangazwa na makatibu wakuu wa vyama hivyo viwili, Yusufu Makamba (CCM) na Maalim Seif Sharif Hamad,” alisema Kapteni Chiligati.
Alisema awali CCM ilipokea mapendekezo yote yaliyotolewa na chama cha CUF na kuyakubali kwa asilimia 95, lakini kukawa na baadhi ya vipengele ambavyo CCM haikuridhika navyo na ndio maana iligoma kusaini makubaliano ya muafaka.
Chiligati alitaja vipengele vilivyochelewesha kumalizika kwa mazungumzo hayo kuwa ni kuondolewa kwa kipengele cha kuwashirikisha wananchi kupiga kura kuhusu serikali ya mseto, kuwepo kwa Baraza la Usuluhishi, kutathimini mwenendo wa Serikali kila baada ya miaka mitano na mchakato wa kuwateuwa mawaziri kulingana na wingi wa wabunge.
Alisema kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kilichofanyika mjini Butiama mkoani Mara kiliyaweka bayana masuala hayo na kuyarudisha kwa Katibu Mkuu wa CUF ili yajadiliwe, kwa kuwa yasingeweza kuimarish utawala bora.
“NEC ilimuagiza Katibu Mkuu kuyafikisha mambo hayo upande wa pili na kutekeleza, hivyo tunashukuru wenzetu wamekubali turudi kwenye meza ya majadiliano.” alisema Kapteni Chiligati.
Alisema awamu hii ya mazungumzo, itaenda sambamba na marekebisho ya Katiba ya Zanzibar endapo pande mbili zinazoshiriki mazungumzo hayo zitakubaliana na kusaini mapendekezo ya muafaka huo yatakayoanza kutekelezwa mwaka 2010.
"Marekebisho ya Katiba pia yatagusa mabadiliko katika sheria ya tume ya uchaguzi ili kwa pamoja viweze kwenda sambamba na mabadiliko ya uongozi wa mseto," alisema.
Alisema jambo lingine ambalo litafanyika ni kuhakikisha kuwa wananchi wanaelimishwa kuhusu taratibu na kanuzi za utawala wa Serikali ya Mseto ili itakapoanza kusitokee tena usumbufu.
Chiligati alisema anaamini mchakato huo utafanyika kwa kasi ili kuondoa kero ya mwafaka inayogubika siasa za Zanzibar sasa.
Gazeti hili lilipowasiliana na Msaidizi wa katibu Mkuu wa CUF mara baada ya Chiligati kusema hayo, alisema chama chake hakina taarifa kuhusu suala la hilo.
"Taarifa hizo sio za kweli, CUF hatuna taarifa wala haijawasiliana na CCM kuhusu suala la mwafaka tangu kimalize mkutano wake wa NEC," alisema.
Jusa alisema CUF hakina taarifa ya kuanza kwa mazungumzo hayo yanayodaiwa kuwashirikisha makatibu wakuu wa CUF na CCM na hata kama ingekuwa na taarifa hiyo bado isingekubali mazungumzo hayo yarudishwe kwenye Kamati ya makatibu wakuu.
"Nani alisema hayo? Sisi hatujapata taarifa ya mdomo wala maandishi. Lakini hata kama tungepata, msimamo wa CUF sasa ni kwamba, mazungumzo hayo yamemalizika kwenye ngazi ya kamati na sasa yanatakiwa kufanywa na viongozi wakuu wa vyama hivyo yaani, Maalim Seif na Karume kwa upande wa Zanzibar au Jakaya Kikwete na Profesa Lipumba," alisema.
Alisema anaamini CCM imetoa kauli kama mwendelezo wa propagansa zake kuhusu mwafaka na kamwe CUF haitakubali kutumika kwa faida ya CCM. |