Burudani
Makala
Habari nyingine
Hadithi
Kolamu
Maoni ya wasomaji
Habari na Picha
Nafasi za kazi
Kona ya Marafiki
 
 
 
Date::11/16/2009
Simba bwana! We acha tu,yashinda 3-1, Yanga, Prisons leo
Wachezaji wa timu ya Simba wakishangilia moja ya goli walilolifunga dhidi ya Mtibwa Sugar.Simba ilishinda magoli 3-1

Dorice Maliyaga

SIMBA imetegeneza historia mpya kwa kushinda mechi zote 11 za mzunguko wa kwanza na kufikisha pointi 33 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku watani zao Yanga leo watakuwa wakijiuliza mbele ya Maafande wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Uhuru.

Mabao ya Mussa Hassan Mgosi, Uhuru Selemani na David Naftari yalitosha kuipa Simba ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mgosi aliunganisha kwa umakini pasi ndefu aliyopewa na kipa Juma Kaseja na kufunga bao la kwanza kwa vijana hao wa Msimbazi katika dakika ya 20.

Mtibwa Sugar watajilaumu wenye kwa kushindwa kuwa makini kwenye ulinzi wakati mchezaji wao Sudi Abdalah alipoangushwa kwenye eneo la penalti, lakini mwamuzi akasema mpira uendeele ndipo Kaseja aliporusha kwa mkono mpira mrefu na kumkuta Mgosi aliyefunga bao hilo kwa shuti.

Winga wa zamani wa Mtibwa, Uhuru Selemani aliyesajiliwa kwa mizengwe mikubwa mwanzoni mwa msimu huu alifungia Simba bao la pili katika dakika ya 49 kipindi cha pili akimalizia kazi nzuri ya Ramadhani Chombo 'Redondo'.

Mabingwa wa Kombe la Tusker walirudi mchezoni na kupata bao la kusawazisha dakika 56 kupitia kwa Yusuf Mgwao aliyeingia kutoka benchi akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Shabani Nditi na kugonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya kumaliziwa na mfungaji.

Vijana hao wa Manungu walifunga bao la pili dakika 70 lililofungwa na Omar Matuta, lakini mwamuzi Dominik Nyamisama kutoka Dodoma alilikataa kwa madai mfungaji huyo alikuwa ameotea.

Vijana wa Mzambia Partick Phiri wakionyesha wamedhamiria kutwaa ubingwa msimu huu waliandika bao lao la tatu dakika ya 86 kupitia kwa Naftari aliyefunga akiunganisha krosi ya Emmanuel Okwi.

Awali mwamuzi Nyamisama aliyakataa mabao mawili ya Simba yaliyofungwa katika kipindi cha kwanza na Mgosi dakika ya kwanza pamoja na lile la Emmanuel Okwi (18) kwa madai wafungaji hao wameotea.

Kocha wa Simba, Phiri amesema ameridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake hususani Naftari na Okwi.

Naye Salum Mayaga wa Mtibwa amewalalamikia waamuzi kuwa ndiyo wanaoharibu soka ya Tanzania kwa kuonyesha upendeleo kwa timu kubwa za hapa nchini.

Leo mabingwa watetezi Yanga watashuka dimbani wakiwa na wazo moja tu la kutaka pointi tatu na kurudi kwenye nafasi ya pili ya msimamo wa ligi hiyo.

Yanga inayofundishwa na Mserbia Kodistan Papic wanajua kwamba kufungwa kwao kutamaanisha watakuwa wamejiweka njia ya panda ya kutetea taji lao.

Timu ya Prisons iliyoanza msimu huu kwa kusuasua nayo inahitaji ushindi kwa hali na mali ili kurudisha matumaini yake ya kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao.

Facebook
        Contact Us DISCLAMER
Email:webmaster@mwananchi.co.tz © Mwananchi Communications Ltd 2006-