Burudani
Makala
Habari nyingine
Hadithi
Kolamu
Maoni ya wasomaji
Habari na Picha
Nafasi za kazi
Kona ya Marafiki
 
 
 
Date::10/31/2009
Sitta: Mwakyembe ana kinga kutohojiwa Takukuru
Na Kizitto Noya

SPIKA wa Bunge Samuel Sitta amemtetea Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe kwamba, ana haki ya kutokubali kwenda katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhojiwa kwa kuwa sheria na kanuni za Bunge hazimlazimishi.

Spika Sitta alitoa kauli hiyo jana alipotakiwa na Mwananchi Jumapili kueleza endapo ni sawa au sio sawa mbunge huyo kugomea wito wa Takukuru unaolenga kumhoji kwa tuhuma za kupokea posho mbili.

Alisema tofauti na makosa mengine ya jinai anayoweza kufanya mbunge kwa sababu zake binafsi, mbunge hawezi kuhojiwa kwa suala linalohusiana na wadhifa wake bila Spika wa Bunge kuwa na taarifa.

"Mbunge akimchoma mtu kisu baa anaweza kukamatwa na spika anapewa taarifa tu, lakini mbunge hawezi kuhojiwa kwa tuhuma za makosa anayodaiwa kufanya kwa mujibu wa wadhifa wake bila spika kufahamishwa kwanza," alisema na kuongeza:

"Hili limewekwa ili kulinda uhuru wa Bunge, kwamba Bunge lishirikiane na mamlaka zingine katika masuala yanayowahusu wabunge. Vinginevyo, kama wabunge watakuwa wanakamatwa kiholela hivi, kazi za Bunge haziwezi kufanyika."

Akifafanua zaidi suala la Mwakyembe alisema: "Yeye ni mwanasheria na huenda amelifahamu hilo, lakini suala lake lina mambo mengi zaidi; atajihakikishiaje haki kwenye kamati ambayo hatujui inamwitia nini? Au anaweza kujihakikishiaje haki kwenye taasisi ambayo bosi wake ana mvutano naye na suala lao halijafikia mwisho kimaamuzi?"

Ingawa Spika Sitta hakutaja aina ya mvutano na jina la bosi anayevutana na Dk Mwakyembe, uhusiano wa mbunge huyo na Takukuru umedorora baada ya kamati yake ya Bunge iliyoundwa kuchunguza zabuni tata ya Richmond, kumtuhumu Dk Edward Hosea ambaye ni Mkurugenzi wa Takukuru kwamba, anahusika na suala hilo kwa vile alishindwa kubaini mianya ya rushwa katika suala hilo.

Awali, baada ya kusikia kwamba, wabunge wanapinga kuhojiwa, Hosea alisisitiza kuwa lazima watahojiwa na kwamba, hakuna mtu aliye juu ya sheria.

Dk Mwakyembe mwenyewe wiki hii alikaririwa na vyombo vya habari akisema hawezi kwenda kuhojiwa na Takukuru kwa vile hatua hiyo ni mbinu za kutaka kuwaziba midomo wabunge.

Hadi jana taarifa za ndani kutoka Takukuru zilieleza kuwa mbunge huyo hajafika kwenye ofisi hizo kuitikia wito wa taasisi hiyo.

Spika Sitta alisema, ni unafiki kuhoji uhalali wa wabunge kuchukua posho za semina leo wakati suala hilo lilikuwapo tangu wakati Tanganyika inapata uhuru.

Hata hivyo, alisema kama ni lazima kuhoji suala hilo, ni vyema ukaandaliwa mchakato wa kisheria ili suala hilo lianze kupigwa marufuku kuanzia sasa.

"Lakini mimi niseme kwamba, ni unafiki kuhoji posho za wabunge leo, posho hizo zilikuwapo tangu miaka ya 1970 mimi nikiwa bado mdogo kabisa, kama tukitaka tuanze upya leo.

Siku zote imekuwa ikielezwa na ndivyo ilivyo kwamba, semina ni kitu kingine na posho ya ubunge ni kitu kingine. Wale wenye semina wanakuja na posho wakijua kuwa hii ni kazi nyingine kwa wabunge," alisema.

Facebook
        Contact Us DISCLAMER
Email:webmaster@mwananchi.co.tz © Mwananchi Communications Ltd 2006-