Burudani
Makala
Habari nyingine
Hadithi
Kolamu
Maoni ya wasomaji
Habari na Picha
Nafasi za kazi
Kona ya Marafiki
 
 
 
Date::3/7/2009
Tanesco yasusa mitambo ya Dowans
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dk Idris Rashid akiondoka mara baada ya kutoa tamko la kuachana na mpango wa shirika hilo kununua mitambo kufua umeme ya DOWANS na kukataa kuulizwa maswali na waandishi wa habari.
YASEMA ISILAUMIWE KWA YATAKAYOTOKEA

Jackson Odoyo

SHIRIKA la Umeme (Tanesco) jana lilitanga kufuta mpango wake wa kununua mitambo ya mitumba ya kuzalisha umeme wa dharura ya kampuni ya Dowans Tanzania Limited, likisema lisibebeshwe lawama kwa yatakayotokea.

"... na wananchi wa Tanzania watafanya maamuzi yao hapo ambapo nchi itakapokuwa imegubikwa na kiza, mahospitali hayatoi huduma; viwanda havizalishi, wanafunzi vyuoni wanashindwa kusoma kwa sababu tulishindwa kufanya maamuzi," alisema mkurugenzi wa Tanesco, Dk. Idrissa Rashid katika mkutano aliouitisha na waandishi wa habari jana.

Uamuzi huo umekuja siku mbili baada ya spika wa Bunge, Samuel Sitta kueleza kuwa msimamo wa kamati ya Nishati na Madini iliyoshauri mitambo hiyo isinunuliwe ndio msimamo wa chombo hicho cha kutunga sheria na hivyo kumaliza mvutano uliokuwepo kati ya kamati hiyo na ile ya hesabu za mashirika ya umma, inayoongozwa na Zitto Kabwe.

Serikali na Tanesco zilikuwa zinataka mitambo hiyo yenye uwezo wa kuzalisha megawati 100 za umeme inunuliwe kwa ajili ya kulinusuru taifa na tatizo linalobashiriwa la upungufu wa umeme, ambao Tanesco inadai mahitaji yake yanaongezeka kwa kasi, wakati uzalishaji ni mdogo.

Katika mkutano wake na waandishi jana, Dk. Rashid alisema kuwa mwelekeo wa suala hilo unaonekana kulipeleka shirika lake kwenye ugomvi wa wanasiasa, jukwaa ambalo alisema hawana mamlaka nalo.

"Ni maoni yetu kwamba tumewasilisha suala hili kwenye ngazi zote kwa ukweli thabiti ambao umezingatia hali halisi ya sasa na inayotarajiwa," alisema gavana huyo wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

"Tunaamini kuna hali inayozuia kuwa na mjadala wa uwazi na ukweli kuhusu masuala haya yenye msingi wa utaalamu. Masuala ya taaluma na ufundi, yanamezwa na hoja za kisiasa. Hali hii haina maslahi yoyote kwa mazingira haya tunayokabiliana nayo wala kwa shirika la Tanesco."

Mkurugenzi huyo alisoma uamuzi huo wa Tanesco wa kurasa tano na baada ya kumaliza alisimama na kuanza kuondoka, akikataa kujibu maswali juu ya taarifa hiyo, ambayo awali ilikuwa isomwe juzi, lakini Tanesco ikaahirisha mkutano huo na waandishi bila ya kueleza sababu za uamuzi huo.

Kuhusu suala hilo kugubikwa na hoja za kisiasa, Dk. Rashid alitoa mfano wa kauli za kiongozi mmoja ambaye alisema alinukuliwa kwenye vyombo vya habari akisema kuwa jitihada hizo ni za "kuwasafisha mafisadi, ni kukiuka taratibu na sheria za nchi".

"... na mwingine alisema akipatiwa fedha, anaweza akapata mitambo mipya ya uwezo huu ndani ya wiki chache tu. Hizi ni kauli zinazopotosha ukweli wala hazizingatii utaalamu bali zimejaa utashi wa kisiasa zaidi na zinachangia kuwavunja mamia ya wafanyakazi wa Tanesco ambao wanafanya kazi kubwa usiku na mchana kuhakikisha nkuwa nchi inapata umeme wa uhakika," alisema Dk. Rashid.

"Sisi si wanasiasa, wala hatufanyi kazi zetu kwa kuweka mizani au kuangalia upepo wa kisiasa. Ni jambo la huzuni kwamba miongoni mwa wanaotoa hoja za kupotosha umma, wengine amepata nafasi ya kukaa nasi na kubadilishana nasi mawazo juu ya hali ya umeme.

"Mara zote Tanesco tumeeleza kwamba tuko tayari kupokea maekezo ya wizara na kamati za Bunge kama taasisi za usimamizi na za uwakilishi wa wananchi."

Dk. Rashid alisema hali ya mvua, ambayo ni chanzo kikubwa cha umeme kuliko vyanzo vingine vyote na wenye unafuu kuliko vyote, si ya kuridhisha. Kulingana na utabiri wa hali ya hewa, mvua za mwaka huu hazitalingana na viwango vya kawaida.”

"Tayari mvua zilizonyesha kwenye mikoa ya Mbeya na Iringa, ambayo ndiyo vyanzo vikuu vya maji ya Mtera, ilikuwa ya kiwango cha chini na katika maeneo mengine mvua zimesimama. Hali hii ilisababisha Tanesco kufanya tathimini ya kina kwenye ngazi zote na baadaye menejimenti ikaiomba bodi ya wakurugenzi kulifikisha suala hili wizarani," alisema Dk. Rashid.

Kuhusu uamuzi huo kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma, Dk. Rashid alisema: "... hakuna wakati wowote ule, ambapo Tanesco imesema kwamba hatua za kununua mitambo hiyo hazitazingatia taratibu husika au nyinginezo zinazofanyiwa kazi kuhusu tuhuma za ukiukwaji wa taratibu za kukodi mitambo hiyo hapo awali.

"Tunashangaa kwa nini watu wenye ufahamu mkubwa sana, wanachanganya mambo haya mawili. Ukweli ni kwamba hoja ya kunua mitambo haijahusisha masuala haya mawili tofauti."

Alisema kabla ya kufikia uamuzi huo, Tanesco ilifanya tathmini ya hali ya mvua na kwamba utabiri wa hali ya hewa unaonyesha kuwa mvua za mwaka huu hazitalingana na viwango vya kawaida.

Alisema baada ya tathmini hiyo, Tanesco ilipeleka ombi la kununua mitambo hiyo serikalini kwa kuwa manunuzi ya mitambo hii haikuwa ni ufumbuzi kamili bali ili kuwa ni ushauri ili serikali na Tanesco wakae na kubaini mpango wa haraka kuhusu uzalishaji wa nyongeza inayoingia kwenye mtandao kwa kiasi cha megawati zisizopungua 200.

Alifafanua kuwa walitarajia kuingiza megawati hizo kwenye mtandao katika kipindi cha miezi 24 ijayo ili umumu huo umeingia kwenye mfumo kabla ya Desemba 2010 na ikiwa ni ziada ya megawati 105 zinazotarajiwa kuingia baada ya kumiliki mitambo ya Dowans.

"Hatua hizo zilikuwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba megawati 45 za Tegeta, megawati 200 za Kiwira zinaigia kwenye mtandao na ikibidi serikali iongeze nguvu kwenye uzalishaji. Tulifanya hivyo tukitambua mazingira ya ukodishaji wa mitambo hiyo, lakini pia tulizingatia wajibu wetu wa kufanya tathmini ya masuala mapana zaidi yanayohusu mitambo hiyo ikiwa ni pamoja na ubora wake," alisema Dk. Rashid.

Kuhusu unafuu wa mitambo, Dk. Rashid alisema "unafuu ulizingatia muda wa kuipata mitambo hiyo kwa kuwa kuangalia muda wa kununua, kupokea, kufunga na kuanza kuitumia wakati mitambo ya kununua kutoka kwa wazalishaji huchukua muda mrefu".

Alitoa mfano wa mitambo ya Wartsila inayozalisha umeme wa megaawati 100 ambayo alisema ilichukua muda wa miezi 18 kabla ya kuanza kazi Novemba mwaka jana.

Uamuzi huo wa Dk Rashid umekuja siku moja baada ya kikao kilichokuchukua saa nne kati yake na naibu wa Waziri wa Nishati na Madini ambacho kilifanyika juzi makao makuu ya shirika hilo. Kabla ya kumalizika kwa kikao hicho, Tanesco iliita waandishi wa habari ili kutoa taarifa mwishoni, lakini mkutano huo na waandishi ukaahirishwa.

Sakata la Dowans limetawala kwenye vyombo vya habari kwa muda sasa baada ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuionya serikali katika nia yake ya kununua mitambo hiyo baada ya kubaini kuwa ilikuwa ikiendelea na mchakato.

Baadaye, Waziri wa Nidhati na Madini, William Ngeleja alitangaza uamuzi wa serikali kukubaliana na ushauri huo wa bunge huku akisisitiza umuhimu wa kununua mitambo hiyo.

Lakini siku chache zilizopita serikali ililikimbizia suala hilo kwenye Kamati ya Mahesabu ya Mashirika ya Umma, ambayo mwenyekiti wake, Zitto Kabwe alitangaza wazi kuwa anakubaliana na mpango huo kwa kujali maslahi ya taifa.

Zitto alisema iwapo Sheria ya Manunuzi ya Umma ndiyo kikwazo katika mpango huo, basi haina budi kubadilishwa kwa kuwa sheria si msahafu.

Kauli yake ilisababisha mabishano zaidi kiasi cha mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, William Shelukindo kudiriki kumuelezea Zitto kuwa anajifunzia kazi Bungeni na kwenye kamati.

Harrison Mwakyembe, mbunge wa jimbo la Kyela na makamu mwenyekiti wa kamati ya Shelukindo, ndiye aliyekuja juu zaidi aliposema kuwa jitihada za Tanesco na serikali zinalenga kuwasafisha mafisadi na kuongeza kuwa ni ni bora nchi iingie gizani kuliko kununua mitambo ya Dowans.

Spika wa Bunge, Samuel Sitta ndiye aliyeonekana kuandaa mazingira ya kuufunga mjadala huo wakati alipoishauri serikali kutonunua mitambo ambayo iliingia kwa utata na ambayo mmiliki wake amefungua kesi dhidi ya mnunuzi mtarajiwa.

Sitta pia alisema Kamati ya Zitto haikustahili kupokea maombi hayo ya serikali ya kutaka ushauri juu ya nia hiyo ya kununua mitambo ya Dowans kwa kuwa hizo si shughuli zake na kwamba ushauri wa Kamati ya Shelukindo ndio msimamo wa Bunge.

Dowans ilirithishwa mkataba wa kuzalisha umeme wa dharura mwaka 2006 baada ya kampuni iliyoshinda zabuni hiyo, Richmond Development Company LLC kushindwa kuleta mitambo hiyo na baadaye kukumbwa na kashfa ya ushindi wa zabuni hiyo uliosababisha Edward Lowassa kujiuzulu wadhifa wake wa waziri mkuu na baadaye kufuatiwa na mawaziri wawili.

Facebook
        Contact Us DISCLAMER
Email:webmaster@mwananchi.co.tz © Mwananchi Communications Ltd 2006-