
| Misaada ya wahisani hurutubisha ufisadi nchini | Send to a friend |
| Tuesday, 21 February 2012 20:16 |
|
MISAADA inayoendelea kutolewa na wahisani kwa Serikali ya Tanzania imetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la vitendo vya ufisadi na ukiukwaji wa haki za binadamu huku ikiwaacha wananchi wakiishi katika maisha duni na umasikini wa kutupwa. Madai hayo yamewekwa bayana na Jarida la The London Evening Post, la Februari 20 mwaka huu ambapo limeeleza kuwa wakati rushwa na ufisadi vikiwa vimeenea katika ngazi zote za Serikali nchini Tanzania, nchi wahisani zimeendelea kuimwagia sifa serikali ya Tanzania. Makala katika Jarida hilo inaeleza kuwa kuitaja Tanzania kama mfano wa kung’ara katika utawala bora na hadithi za mafanikio kwa Afrika ni jambo linaloacha maswali mengi. Jarida hilo linaeleza kuwa uwanja wa kisheria nchini Tanzania umekuwa kama sinema fupi ambapo ufisadi, rushwa na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu umehalalishwa na kukubalika kuwa si changamoto ya kupewa kipaumbele huku haki ikinunuliwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya matajiri na wenye nguvu wakati maskini wakipuuzwa na kudhalilishwa. Mbaya zaidi, sinema hiyo inafadhiliwa na nchi wahisani, ambazo zinaendelea kumwaga misaada kwa Tanzania na kuitaja Tanzania kama hadithi ya mafanikio Afrika huku wakishindwa kutambua kuwa misaada hiyo ndio nguzo kubwa ya ufisadi nchini. “Pamoja na ushahidi uliopo kwa kuwepo ufisadi unaoibuliwa kila mara nchini Tanzania, nchi wahisani zinaonekana kujitia upofu, ama kufumbia macho kwa makusudi matukio yanayoonyesha ukosefu wa utawala bora na kuongezeka kwa vitendo vya rushwa na ufisadi hasa katika taasisi zenye mamlaka ya kutoa haki kama vile polisi na mahakama” inaeleza sehemu ya Jarida hilo. Januari mwaka huu, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Corner Diane alithibitisha kuwa Uingereza imekuwa ni mwekezaji mkubwa nchini Tanzania. "Kuna nchi nyingi barani Afrika ambapo sisi tunawekeza lakini hii ni nchi bora kwa ajili ya biashara na uhusiano wa kiuchumi, kama washirika wa maendeleo, Uingereza kihistoria imekuwa mtoaji mkubwa wa misaada kwa Tanzania ambapo mpango wetu wa kutoa misaada umeongezeka zaidi,” inaeleza sehemu ya Jarida hilo. Inashangaza kuona nchi wahisani zikichekelea matumizi hayo mabaya ya misaada kwa kuendekeza rushwa na wimbi kubwa la ufisadi, jambo linalojenga hoja juu ya maadili, utawala bora na utawala wa sheria ambavyo vyote vimeonekana kuwekwa pembeni na viongozi wa Serikali ya Tanzania. Taarifa hiyo inasema kuwa wahisani walipaswa kuchangia na kushiriki kikamilifu katika mapambano ya rushwa na ufisadi kwa kuweka msisitizo kwenye utawala bora hasa kutokana na kuwepo kwa mfumo na maendeleo duni kisheria yanayotoa kinga ya kisheria dhidi ya wala rushwa na mafisadi. Uwajibishwaji wa mafisadi umekuwa na hadithi isiyokuwa na mwisho hasa kwa kutokuwepo kwa nguvu ya ziada inayoshinikiza uwajibishwaji huo ambao kimsingi nguvu hiyo ilipaswa kutoka kwa nchi wahisani kwa kukemea matumizi mabaya ya misaada wanayotoa jambo ambalo lingeweza kuchukuliwa kwa uzito unaostahili. |

Habari Mpya
Picha
Zenye Mvuto
- Prof Mwandosya aapishwa waziri kazi maalum
- Katiba Mpya: Wananchi Makambako waapa, iwe jua au mvua lazima watoe maoni yao
- Mchakato wa Katiba: Nahodha yupi aaminike? 1
- Wanavyosema wanasiasa kuhusu Katiba mpya
- Serikali inasita nini kutumia Kiswahili kufundishia shule za sekondari?
- Jamii inaweza kuleta mabadiliko katika elimu
- Nafasi za Kazi
- Links za wateja na washirika wetu
- Muswada wa madini waitoa jasho serikali
- Bi kizee asafari kilometa 50 kupinga hotuba ya JK, AMUONYA ASITUMIE MADARAKA YAKE VIBAYA
- Mishahara sekta binafsi Tucta yashtukia danganya toto
- Vigogo UVCCM wajiuzulu
- Mwinyi atetea ajira za wafanyakazi, ashauri utu uheshimiwe kudumisha Amani















Comments
Wenye fedha ndio wenye haki katika nchi hii ambayo askari polisi anaamua tu kuwafyatulia risasi za moto wananchi wasio na silaha yoyote mnkononi na kuwaua na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi yake!!