
| Mbunge apinga tamko la Wizara kuhusu Studio za THT | Send to a friend |
| Monday, 17 January 2011 12:39 |
Mwandishi WetuSAKATA la Studio aliyotoa Rais Jakaya Kikwete limechukua sura mpya baada ya Mbunge wa Mbeya mjini kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo 'CHADEMA' Joseph Mbilinyi kudai kuwa anashangazwa na tamko lililotolewa na Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo kuhusu studio hiyo ambayo Wizara imedai kuwa ilitolewa na Rais Jakaya Kikwete kufuatia ombi binafsi la Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Tanzania House of Talent (THT). Mbilinyi ukipenda unamuita Mr Two au Sugu alisema yupo tayari kula kiapo kuhakikisha haki inatendeka katika suala hilo na atalifikisha bungeni kwa kuwa tamko la Wizara limelenga kulinda watu wachache, walionufaika na mamilioni yaliyotolewa na Rais Kikwete kwa ajili ya wasanii huku wakiwakandamiza wasanii ambao ni walengwa. Kauli ya mheshimiwa Sugu imekuja siku mbili baada ya Wazira ya Habari Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi kutoa tamko mwishoni mwa wiki ikieleza kuwa Studio iliyotolewa na Rais ni ombi binafsi la THT, ambalo ilimuomba rais wakati alipohudhuria sherehe zao za kutimiza miaka mitatu Desemba 8 mwaka 2008. "Kwa kutumia jukwaa la sherehe hizo risala mbili tofauti zilisomwa moja ikiwa ni ya THT na nyingine Lady Jay Dee akiwakilisha wasanii 20 walioudhuria sherehe hizo kama Afande Sele, Dully Sykes, Banana, Keisha, Fela, Chege, Temba na Bushoke, risala zote mbili zilikuwa na maombi 11 na mahususi ilikuwa ni kununuliwa studio ya mastering,"ilieleza taarifa hiyo ya Wizara. "Rais aliyasikia maombi yote na kuahidi kuwanunulia studio hiyo iwapo wasanii watakuwa na umoja wao kwa ajili ya kupanga mipango mirefu ya kuendesha studio hiyo na kuhakikisha inakuwa si kichocheo cha chuki na ugomvi kati ya wasanii na kupendekeza Ruge Mutahaba, aliyekuwa ndio mwenyeji wa shughuli hiyo abebe jukumu la kuhakikisha hayo yanafanyika,"ilieleza taarifa hiyo. Taarifa hiyo pia ilieleza,"baada ya sherehe mchakato wa kuunda umoja ulifanyika ikaundwa Tanzania Fleva Unit mwenyekiti akiwa Lady Jay Dee na mpaka sasa hakijasajiliwa na sekretarieti hiyo imeendelea kutoa taarifa za hatua mbali mbali za maendeleoo ya mpango kazi wao kwenye ofisi ya rais ambayo imeendelea kuwasaidia katika hatua nyingine kama vile kusaidia kupatikana kwa fedha za pango, kusaidia kutafuta mtaalamu wa kufunga na kuendesha studio ikiwemo kufundisha vijana wa Tanzania." "Sekretarieti inakamilisha mchakato mzima wa kujiandikisha kama chama na pia kama taasisi ya kibiashara, kwani sababu kuu ya studio kuwepo ni kutumika kibiashara,"iliongeza taarifa hiyo ya Wizara. Lakini jana Mbilinyi aliiambia Mwananchi kuwa,"Wizara imekurupuka, wao wametengeneza lugha ya kisiasa kuzuga Watanzania na wasanii, lakini nitahakikisa haki inatendeka, wahusika wote wa ufisadi huu wa wasanii wanachukuliwa hatua zinazostahili, kwa maana hizo milioni 225 zinazotolewa na Rais zinalipa nyumba hilo ni nyumba ya kina nani na kama rais alitoa studio kwa mtu binafsi yaani THT, je wanaikabidhi vipi tena kwa Fleva Unity?,"alisema kwa kuhoji. Alisema,"Rais (Kikwete) aliposema anasaidia wasanii, cha kushangaza kigogo ambaye ana nguvu mpaka serikalini akaenda Basata na kusajili chama cha Wasanii wa Bongo Fleva, 'Tanzania Fleva Unit', tunajua na tuna uhakika hizo fedha zilitolewa kwenda Chama cha Wasanii wa Kizazi kipya (TUMA)' kwa ajili ya kusaidia wasanii na si kwa ajili ya kulipa pango kama Wizara inavyojaribu kutuambia na hazijatoka kwa jina la Fleva Unit zimetoka kwa jina la TUMA." "Halafu cha kushangaza wanajifanya Fleva Unit hakijasajiliwa wakati nina uhakika kimesajiliwa nipo tayari kula kiapo mimi mwenyewe nilimuuliza mzee Ruhala (Angelo - Mtafiti wa Utamaduni Basata) kwa nini mnasajili chama kingine wakati kile cha zamani kipo jibu alilonipa,...Bwana eee tumeshinikizwa toka juu," alisema Mbunge huyo wa Mbeya. Viongozi wa TUMA ambayo iliundwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata ) mwaka 2004 chini ya uenyekiti wa Fred Maliki, maarufu Mkoloni, mwekahazina, Hazma Mpondela, katibu prodyuza wa muziki anayefahamika kwa jina la Brayton, wajumbe ni Rado Haule, Stara Thomas na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi. "Katiba ya TUMA kuna kipengele kinasema TUMA ndio chombo pekee ambacho kinasimamia wasanii wa kizazi kipya na ndicho chombo pekee ambacho kitapokea misaada kutoka ndani na nje ya nchi,"alisema Mbilinyi. Alisema," nilimuuliza Ruhala kuhusu kipengele hicho kuwa hawaoni wamefanya kosa kusajili chama kingine wakati kile kipo na kama walishinikizwa kwa nini hawakutushirikisha ili kama ni kubadilisha baadhi ya vipengele kwenye katiba yetu tubadilishe ili wao wawe huru kusajili chama kingine, hakuwa na jibu. Mbilinyi alisema,"lile faili la usajili wa chama cha Fleva Unit pale Basata wanajifanya limepotea ili ijulikane Fleva Unit hakikusajiliwa kama Wizara inavyodai, huu ni ubabaishaji. |



Mwandishi Wetu











Comments