YALIYOJIRI 2019: Waraka wa Makamba, Kinana gumzo, mali za Mbowe zapigwa mnada

Dar es Salaam. ‘Harufu’ ya waraka wa Makatibu wakuu wawili wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana, iliyoanza kusambaa Julai 14, ilichafua hali ya hewa kwa mfululizo wa siku kadhaa ndani na nje ya chama hicho kinachoongoza Serikali.
Kupitia waraka huo waliouwasilisha kwa Katibu wa Baraza la Ushauri la viongozi wakuu wastaafu katika CCM, Pius Msekwa, Makamba na Kinana walikuwa wakilalamika kudhalilishwa kwa uzushi na uongo uliofanywa na mtu aliyejitambulisha kuwa mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.
Julai 15, Msekwa alifunguka wazi kuhusu madai ya vigogo hao kabla ya siku tatu baadaye kuwajibu kwa maandishi akiahidi madai yao kushughulikiwa ngazi ya juu ya chama. Wakati huo makada na viongozi wa chama hicho wakipinga uamuzi wa wastaafu hao hadharani licha ya wanazuoni kuwaunga mkono.
Waraka huo uliendelea kuwa gumzo ukiibua mijadala huku baadhi ya watu waliokuwa wakijadili wakidai ulitishia kukipasua chama huku wachambuzi wa duru za kisiasa wakimtaka mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli kutoa neno huku Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ali akitoa onyo kwa makundi yaliyohatarisha uhai wa chama.
Hadi kalenda ya Julai inafungwa, harufu ya sakata hilo haikuwa imemalizika kwani hivi karibuni wastaafu hao Kinana, Nape na mwingine Membe wanasubiri wito wa kujieleza mbele ya vigogo 12.
Katika mwendelezo wa shina la waraka huo, Januari Makamba na Nape Nnauye walinaswa kupitia sauti za simu wakimpiga kijembe Rais Magufuli. Wengine katika sauti hizo ni Kinana na Yusuph Makamba.
Mawasiliano hayo yalinaswa baada ya kusambaa mitandaoni ikiwa ni siku chache baada ya Rais Magufuli kutengua nafasi ya Januari Makamba aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Julai 21 hivyo kuibua mjadala wa jambo juu ya jambo.
Mwezi wa Afcon
Mjadala mwingine uliovuta hisia kila kona ya mitandao ya kijamii hata kurasa za mbele za magazeti ni pamoja na mdudu wa siasa aliyeingilia Taifa Stars wakati ikishiriki fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) nchini Misri kupitia kundi C lililokuwa na timu za Kenya, Algeria na Senegal.
Stars iliyokuwa na rekodi ya kushiriki mashindano hayo miaka 39 iliyopita, ilitolewa raundi ya kwanza kwa kuchapwa jumla ya mabao manane, ilifungwa 2-0 na Senegal, 3-2 na jirani zao wa Kenya na ikafungwa 3-0 na Algeria.
Matokeo hayo yalizua mijadala iliyowagusa hadi wabunge huku wengine wakimjadili Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ambaye alitangaza kwenda Misri kuiunga mkono timu hiyo lakini hilo halikusaidia kuipa Stars matokeo mazuri.
Jambo lingine lililoibua mjadala baada ya Stars kufanya vibaya kwenye mashindano ni uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumtimua kazi Kocha wa Stars, Emmanuel Amunike.
Maumivu upinzani
Mwezi Julai ulikuwa kama mwendelezo wa maumivu waliyodai kukutana nayo viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani baada ya kuendelea kusota mahabusu kwa kesi za uchochezi pamoja na zuio la mikutano ya hadhara na ile ya ndani.
Kwa upande wa CCM mikutano hiyo iliendelea, mfano Julai 7, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ali alianza ziara mkoa wa Kilimanjaro ili kuongeza nguvu ya chama hicho katika chaguzi zijazo.
Wakati wapinzani wakilalamikia zuio la mikutano ya hadhara, Julai 8, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Simon Sirro Julai 18 walidai kutopokea malalamiko ya viongozi hao kuhusu madai ya hujuma wanazofanyiwa na Jeshi la Polisi wanapotaka kufanya mikutano ya ndani au hadhara jimboni.
Matamko hayo ya IGP na msajili yaliibua mijadala zaidi baada ya viongozi wa upinzani kupinga huku wachambuzi wa duru za siasa wakidai hakuna anayeweza kumaliza changamoto hiyo kati yao.
Julai 30, Rais John Magufuli aliyezuia mikutano ya kisiasa isipokuwa kwenye maeneo ya uwakilishia, alikutana uso kwa uso na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyekuwa amefiwa na ndugu yake Meja Jenerali mstaafu Albert Mbowe, Jijini Dar es Salaam. Haikufahamika kama walizungumza chochote kuhusu hali ya kisiasa nchini.
Wakati huo huo Julai 6, mali za mwenyekiti huyo wa Chadema, zilipigwa mnada. Mali hizo zilizoshikiliwa kwa miaka mitatu ni zile zilizokuwa kwenye ukumbi wa disco wa Bilicanas ambazo mwaka 2016, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lilizichukua kwa madai ya kutolipwa kodi kwa miaka 20.
Nje ya tukio hilo, Tundu Lissu aliyekuwa Ubelgiji akitibiwa majereha ya risasi, aliendelea kuibua mjadala hasa kwenye mitandao ya kijamii baada ya Bunge kumvua nafasi yake ya uwakilishi Singida Mashariki(Chadema).
Matumaini, majonzi
Ukiachana na maumivu ya wanamabadiliko, majonzi yalitanda katika sekta ya habari baada ya wafanyakazi watano wa kampuni ya Azam Media kufariki dunia Julai 8, katika ajali ya gari wakati wakielekea wilayani Chato, mkoani Geita katika uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Chato-Burigi. Ilikuwa ni mshtuko mkubwa.
Mwezi huo pia uliibua mjadala kwa Watanzania baada ya mahakama kuanza kutekeleza agizo la Rais Magufuli aliyetoa pendekezo la kupunguzwa kwa mahabusu.
Hii ni baada ya Julai 17, Rais Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza katika gereza la Butimba, Mwanza na kushuhudia changamoto nyingi ikiwamo msongamano wa mahabusu huku wengine wakiwa wamekaa muda mrefu bila kupelekwa mahakamani na wengine kwa kesi za kubambikiwa.
Siku tano baadaye, Rais Magufuli akaagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) aliyesimamishwa kazi mwaka 2016 kurejeshwa kazini huku mwandishi wa habari, Erick Kabendera akikamatwa Julai 29 na Polisi akituhumiwa kuwa si raia wa Tanzania kabla ya kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.
Hayo ni kwa uchache tu katika matukio mengi yaliyochapishwa katika magazeti ya Mwananchi kati ya Julai mosi hadi 31, 2019.