Serikali ya Tanzania yashindwa rufaa dhidi ya Abdul Nondo

Muktasari:
Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Iringa imemuachia huru aliyekuwa mwenyekiti wa mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo baada ya kushinda rufaa iliyofunguliwa na Serikali ya Tanzania kupinga uamuzi wa hukumu aliyoshinda Novemba 5 mwaka 2018.
Iringa. Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Iringa imemuachia huru aliyekuwa mwenyekiti wa mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo baada ya kushinda rufaa iliyofunguliwa na Serikali ya Tanzania kupinga uamuzi wa hukumu aliyoshinda Novemba 5 mwaka 2018.
Akisoma hukumu hiyo leo Jumatatu Desemba 23, 2019 Jaji Pantelini Kente amesema upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha makosa aliyotuhumiwa nayo mtuhumiwa bila kuacha shaka yoyote na mahakama kuamua kumuachia huru Abdul Nondo.
Nondo alikuwa anashtakiwa kwa makosa mawili, moja ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni, kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma Mafinga.
Novemba 5 mwaka 2018, Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa ilimemuachia huru Nondo kutokana na Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka mawili yaliyosababisha afikishwe mahakamani hapo.
Nondo alifikishwa kwa mara ya kwanza katika mahakama hiyo Machi 21, 2018 akikabiliwa na makosa mawili likiwamo la kuchapisha taarifa za uongo kwamba “nipo hatarini” na kuzisambaza mtandaoni.
Kosa la pili, lilikuwa ni kutoa taarifa za uongo kwa askari Polisi, Koplo Salim wa Kituo cha Polisi Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa kuwa alitekwa na watu wasiojulikana Dar es Salaam na kupelekwa kiwanda cha Pareto mjini Mafinga.
Soma zaidi: Serikali yanena kuhusu Abdul Nondo