Rais wa Afghanstan ashinda kwa muhula wa pili

Rais wa Afghanstan, Ashraf Ghani
Muktasari:
- Wananchi wa Afghanstan wamemchagua Rais Ashraf Ghani wa nchi hiyo kuongoza kwa muhula wa pili wa miaka mitano. Uchaguzi huo ulifanyika Septemba 28 na matokeo yamechelewa kutangazwa kwa sababu ya malalamiko ya udanganyifu na maandamano kutoka kwa vyama vya upinzani.
Kabul. Rais wa Afghanstan, Ashraf Ghani ameshinda kwa muhula wa pili wa miaka mitano baada ya kutangazwa kwa matokeo ya awali ambayo yanaonyesha kiongozi huyo amepata asilimia 50.64 ya kura zilizopigwa Septemba 28 mwaka huu.
Tume Huru ya Uchaguzi (IEC) ilitangaza matokeo hayo jana ikionyesha mshindani wa karibu wa Ghani, Abdullah Abdullah akishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 39.52 ya kura zote milioni 1.9 zilizopigwa katika uchaguzi huo uliokumbwa na maandamano kwa madai ya udanganyifu.
Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Gulbuddin Hekmatyar ameshika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 3.85 ya kura zilizopigwa.
“Tumekamilisha kazi yetu kwa uwajibikaji na uaminifu,” mwenyekiti wa IEC, Hawa Alam Nuristani alisema katika mkutano wake na vyombo vya habari mjini Kabul ambako matokeo ya awali yalitangazwa.
Matokeo hayo ambayo yalipangwa kutangazwa Oktoba 19, yamecheleweshwa mara kadhaa huku IEC ikitoa sababu kuwa ni matatizo ya kiufundi, malalamiko ya udanganyifu na upinzani kutoka kwa wagombea.
Alisema wafuasi wa Abdullah walivunja ofisi kadhaa za uchaguzi sehemu mbalimbali nchini humo wakiwazuia wafanyakazi wa uchaguzi kuhesabu upya kura kwa zaidi ya mwezi.
“Kulikuwa na sababu mbalimbali za kwanini matokeo ya awali yamechelewa,” msemaji wa IEC, Zabih Sadaat aliliambia shirika la habari la Al Jazeera.
“Sababu kubwa ilikuwa ni vyama vya upinzani kufanya migomo na maandamano nje ya ofisi zetu katika majimbo saba. Hatukuweza kufanya kazi yetu,” alisema.
Wakidai kufanyika kwa udanganyifu kwenye uchaguzi huo, timu ya Abdullah jana ilitangaza kwamba haikubali matokeo hayo na kueleza malalamiko yao dhidi ya IEC.