Mradi mkubwa wa maji kutoka Arumeru kuwakomboa wakazi wa Mirerani

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Zephania Chaula akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya kampuni ya Songambele 1999 Ltd, Mji mdogo wa Mirerani. Picha na Joseph Lyimo
Muktasari:
- Kero ya maji Mirerani kumalizika 2020 Wananchi wa mji mdogo wa Mirerani watanufaika na mradi mkubwa wa maji kutoka Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha unaotarajia kutumia gharama ya Sh4 bilioni.
Mirerani. Wananchi wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara wanaokabiliwa na ukosefu wa maji safi na salama kwa muda mrefu, wataondokana na kero hiyo baada ya Serikali kuanzisha mradi wa maji yatakayotoka Mkoani Arusha.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula ameyasema hayo Desemba 29, 2019 mji mdogo wa Mirerani kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya kampuni ya Songambele 1999 Ltd, inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu wa mikoa ya Manyara na Arusha, Dennis Kimario.
Chaula alisema hivi karibuni Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa alitembelea eneo la Valeska mkoani Arusha na kukagua kisima kirefu kitakachopeleka maji safi na salama kwenye mji mdogo wa Mirerani.
Amesema mradi huo mkubwa wa maji unaotarajiwa kugharimu Sh4 bilioni unaotarajia kukamilika mwaka 2020 na awali wameshatenga Sh700 milioni kwa ajili ya kutandaza mabomba ya maji kutoka Valeska hadi Mirerani.
"Changamoto ya maji mnayolalamikia ninyi wawekezaji wa mji wa Mirerani kina Kimario na wananchi kwa ujumla itafikia ukingoni mwaka 2020 kwani serikali ipo kazini," amesema Chaula.
Alimpongeza Kimario kwa kuwekeza mradi mkubwa wa hoteli ya kulala wageni, kuuza vinywaji, vyakula na kutoa ajira kwa wananchi 50 wa mji mdogo wa Mirerani.
"Wawekezaji kama ninyi ndiyo tunawataka kwani mnatoa ajira, mnalipa kodi, sasa nendeni na Orkesumet makao makuu ya wilaya ya Simanjiro mkawekeze pia kwani hoteli ni chache na uhitaji ni mkubwa," amesema Chaula.
Mkurugenzi wa Songambele 1999 Ltd, Dennis Kimario amesema aliandaa maadhimisho hayo ili kumshukuru namna alivyoweza kusimamia biashara zake bila kutetereka.
"Kufanya kazi kwa muda wa miaka 20 siyo jambo dogo ndiyo sababu akaandaa maadhimisho hayo kwenye mwisho wa mwaka 2019 na kupokea mwaka mpya wa 2020 tukijaliwa na Mungu," amesema Kimario.
Paroko wa parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozali Takatifu wa Kanisa katoliki Mirerani, Padri Vincent Ole Tendeu amesema jamii inapaswa kuiga matukio kama hayo kwa kumshukuru Mungu kwa kazi ambazo zinakupatia riziki.
Padri Ole Tendeu amesema ni jambo zuri kumshukuru Mungu na kumshirikisha katika shughuli unazofanya na pia kujitathimini mahali ulipotoka, ulipo na uendapo ili kuona mwelekeo wa hatua unazopiga.