Ambao hamjasajili laini za simu msimamo wa Serikali ya Tanzania uko palepale

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwele
Muktasari:
Serikali yashikilia msimamo wa kufunga laini zisizosajiliwa Desemba 31 wakati ikisaini makubalino ya ujenzi wa jengo la Umoja wa Posta Afrika (PAPU)
Dar es Salaam. Serikali imesisitiza kuwa Desemba 31, mwaka huu itafunga laini zote za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole na haitaongeza muda wa ziada kwa ajili ya zoezi hilo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwele ameyasema hayo leo wakati wa hafla ya uwekaji saini makubaliano ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Umoja Posta Afrika litakojengwa jijini Arusha.
Amesema, “Tarehe 31 tunakamilisha usajili tutakata laini zote ambazo zitakuwa hazisajiliwa,naomba tu niwaambie umuhimu wa hili zoezi, tumefanya hivi kwa sababu watanzania wengi wanaibiwa mtu mmoja anakuwa na laini 100 na kuanza kufanya uhalifu.”
Akizungumzia ujenzi wa jengo hilo litakalogharimu Sh33.5 bilioni, Waziri Kamwelwe amesema litajengwa kwa ushirikiano kati ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Umoja wa Posta Afrika(PAPU).
Shughuli ya utiaji wa saini hizo umefanywa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba na Mkuu wa Operesheni, Teknolojia wa PAPU, Nathan Mkandawile na mkandarasi kutoka China wa kampuni ya Beijing Contruction Company Limited.
Kamwelwe amesema umoja huo ambao unashirikisha nchi 45 za Afrika, umekubaliana kujenga jengo hilo jijini Arusha ambako kutakuwa makao makuu.
Amesema kutokana na umuhimu wa jengo hilo, Serikali itatoa ushirikiano ili kuhakikisha linajengwa kwa ubunifu na ustadi mkubwa na kwa kuanzia Serikali imetangaza kutoa msamaha wa kodi kwa vifaa vyote vitakavyotumika kwa ajili ya ujenzi.
“Ni mradi wenye hadhi kubwa kwa Taifa na Kimataifa ,serikali itasimamia kuhakikisha ujenzi huu unakuwa na ubora na ufanisi mkubwa na unapaswa ukamilike chini ya kipindi cha miaka miwili(miezi 24) unatakiwa uwe umekwisha pamoja na mkanadarasi kupewa miezi 30,”alisema Mhandisi Kamwelwe.
Amebainisha kuwa kwakuwa serikali ipo nyuma ya mradi huo uangalizi utakuwa mkubwa kwakuwa awali ulishindwa kutekelezeka baada ya kuwapo kwa ukwamishaji kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama.
Mhandisi Kilaba h amesema mradi huo ulisainiwa tangu Septemba 2016 lakini uwepo wa vikwazo kutoka katika baadhi ya nchi wanachama umefanya ujenzi huo kuchelewa.
“Ujenzi wa mradi huu ulikuwa na mziengwe mingi lakini kwa sasa mpaka tumefikia hatua yakusaini maana yake tumeweza kushinda vikwazo hivi vya kisiasa ambavyo tuliwekewa na baadhi ya nchi,” alisema Mhandisi Kilaba.