Iliyokuwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji ilikwamisha uzalishaji mazao Katavi - Waziri

Waziri wa kilimo Josephat Hasunga baada ya kufika eneo la mradi wa ujenzi wa skimu Karema akionyeshwa na Mbunge wa jimbo la Tanganyika Moshi Selemani Kakoso ukubwa wa eneo
Muktasari:
Ucheleweshwaji wa ujenzi wa skimu ya umwagiliaji maji katika kata ya Karema Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi uliodumu kwa miaka minane sasa, umesababisha wakulima kushindwa kutimiza ndoto zao za kuongeza uzalishaji mazao.
Katavi. Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema ucheleweshwaji wa ujenzi wa skimu ya umwagiliaji maji katika kata ya Karema Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ulisababishwa na iliyokuwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji uliodumu kwa miaka minane, umesababisha wakulima kushindwa kutimiza ndoto zao za kuongeza uzalishaji mazao.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akizungumza na wananchi hao katika mkutano wa hadhara, uliofanyika Kijiji cha Karema jana Jumapili Desemba 29, 2019 baada ya kukagua mradi huo, amesema tatizo hilo limewaathiri wakulima wengi nchini, kutokana na iliyokuwa wizara ya maji na umwagiliaji kushindwa kukamilisha.
Amesema miradi ya ujenzi wa skimu za umwagiliaji maji nchini iliyotekelezwa na wizara hiyo ukiwemo wa Karema ni 2,678, lakini inayofanya kazi haizidi 30.
“Wizara imevunjwa, hapa mnalo bonde zuri sijawahi kuliona, maji kwa wingi watu wanaweza kulima hata vijana nimeambiwa, naagiza Mhandisi wa mkoa na wilaya mifereji yote iliyosambazwa kwenye mashamba yote ikamilike, siyo mlivyochimba kama mahandaki,” amesema Hasunga.
Akisoma taarifa ya mradi, Ofisa Umwagiliaji wa halmashauri hiyo Yusuph Mukhandy amezitaja changamoto zilizokwamisha kuwa ni uhaba wa fedha kwaajili ya ujenzi wa bwawa kubwa la kuhifadhi maji, ujenzi wa mifereji mikuu na ya matoleo pamoja na usakafiaji.
“Changamoto nyingine ni Fedha za ujenzi wa miradi kuletwa kwa kuchelewa au kutoletwa kabisa na kuwekwa ngazi ya wizara badala ya eneo la kazi,” amesema Mukhandy.
Gervas Kashinji mmoja wa wakulima wa eneo hilo amesema walitoa mashamba yao ili kupisha mradi huo, lakini mpaka sasa hakuna mafanikio waliyoyapata.
“Tumeharibiwa mashamba yetu, kabla ya mradi nilikuwa nazalisha gunia 30 za mpunga, lakini kwa sasa napata 10 tu maji yanakuwa mengi huwezi kulima,” amesema Kashinji.
Ujenzi wa mradi wa skimu ya umwagiliaji Karema wenye ukubwa wa hekta 2, 721 endapo ukikamilika utawanufaisha wakazi 33,977 ambapo hadi sasa umegharimu Sh742,485,000 na unatarajia kukamilika kwa gharama ya Sh4.8 bilioni.