Urasimu kikwazo kikuu cha ustawi wa ushirika

Wanachama wa Mviwata wakifuatilia mhadhara juu ya nafasi ya Ushirik katika Ujenzi wa uchumi wa Kitaifa wakati wa Mkutano Mkuu wa Chama hicho uliofanyika mkoani Morogoro. Picha na mpiga picha Wetu
Dar es Salaam. Baada ya mhadhara uliodumu kwa zaidi ya saa moja kuhusu umuhimu wa ushirika katika ujenzi wa uchumi wa kitaifa, ilikuwa ni wakati mtoa mada kupokea maswali kutoka kwa wakulima na wazalishaji wengine wadogo waliokuwa wanamsikiliza kwa makini muda wote huo.
“Serikali ndiyo imekuwa chanzo kikuu cha kuua ushirika katika nchi hii,” alianza kusema mshiriki mmoja.
“Hili ni lazima likome. Sasa unadhani ni mbinu gani sisi kama wakulima wadogo tunaweza kuitumia kukomesha uharibifu huu wa juhudi zetu za kujikomboa kupitia ushirika?”
Mshiriki mwingine, akidhihirisha jazba isiyo kifani dhidi ya tatizo hilo, alimuomba mkufunzi aishauri Serikali, akisema: “Unaweza kuishauri nini Serikali ili badala ya kuua ushirika katika nchi hii, iusaidie kustawi na kutoa mchango wake stahiki?”
Sabatho Nyamsenda, mwanasayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mkufunzi katika hafla hiyo, alikuwa ndio kwanza amemaliza kuwaeleza washiriki namna ushirika unavyoweza kuwa suluhu ya matatizo mengi tu yanayolikabili taifa kwa sasa, ikiwemo uchumi wake ambao ameuita tegemezi kupitiliza.
Kanuni ya umasikini
“Lengo la mazao tunayozalisha na kuvuna ni kusafirisha nje ya nchi kwa ajili ya kuchakatwa na viwanda vya nje. Na mahitaji mengi tunayotumia, kwa sehemu kubwa, tunaagiza kutoka nje. Huo ni uchumi mgonjwa. Una ugonjwa wa utegemezi,” alisema.
“Uchumi ambao wananchi wanazalisha wasichokitumia na wanatumia wasichozalisha. Na hapo ndipo ilipo kanuni ya umasikini. Kama hamtaki aina hiyo ya uchumi, ni lazima kufikiria mfumo mbadala wa umiliki wa njia kuu za uzalishaji mali. Mfumo ambao nguvu ya uzalishaji inamilikiwa na watu wanaozalisha. Uchumi wa aina hiyo ni uchumi wa ushirika.”
Washiriki wengi katika mkutano huo wa 24 wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata) uliofanyika Morogoro Desemba 12, 2019, walikuwa wanafahamu hilo. Wengi wao tayaru ni wanachama wa ushirika au waliwahi kuwa kabla ya vikundo vyao vya ushirika kufa.
Kwa mtazamo wao, Serikali kuingilia shughuli za ushirika ni kikwazo namba moja katika kukua kwake na hivyo kukwamisha lengo la kujenga uchumi mbadala, uchumi ambao njia kuu za uzalishaji zinamilikiwa na wengi kuliko mtu mmoja.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na zaidi wakulima na wazalishaji wengine wadogo zaidi ya 300 kutoka sehemu mbalimbali za nchi, ilidhihirika kuwa bila ya mabadiliko makubwa katika mfumo na muundo mzima wa ushirika, muundo ambao utapunguza au kuondoa kabisa uingiliaji wa Serikali katika shughuli za ushirika, ni ngumu sana kuutumia ushirika kujenga uchumi wa kitaifa.
“Kuna uhusiano mkubwa kati ya uingiliaji wa Serikali katika shughuli za ushirika na kufa kwa ushirika,” Veronica Sophu, mkulima mdogo kutoka Mbeya, aliiambia Mwananchi pembezoni mwa mkutano huo.
“Hii ni kwa sababu wataalamu wa ushirika wamekuwa wakishirikiana na viongozi wabovu wa ushirika kuhujumu juhudi za wazalishaji wadogo.”
Sophu anawakilisha maoni ya wazalishaji wengi wadogo wanaoonekana kuchoshwa na hujuma dhidi ya ushirika nchini.
Tuhuma za hujuma
Happiness Orono, mkulima mdogo kutoka Mbozi, Mbeya, aliieleza Mwananchi kwamba anawachukia sana maofisa ushirika kiasi kwamba akiwaona anatetemeka. Anasema hii ni kutokana na hujuma zao ndio maana kikundi chao kilikufa.
Kamsamba Amcos, ushirika ambao Orono alikuwa mwanachama, ulifikia hatua ya kuweka stakabadhi ghalani ili baada ya kuweka mazao yao weweze kukopa na kupata fedha za kukidhi mahitaji yao ili bei ikipanda wauze kwa tija.
Walihitaji saini ya ofisa ushirika wa wilaya ambaye aliwaomba rushwa ya Sh1 milioni ili waweze kupata mkopo wa Sh150 milioni. Orono anasimulia kwa masikitiko: “Akataka tuchange milioni moja tumpe. Aliponyimwa rushwa, hakusaini cheki, na hivyo mkopo haukupatikana. Ushirika ukafa.”
Hiyo ni njia moja, lakini kuna nyingine ambayo ilitajwa na wazalishaji wadogo inayoua ushirika. Hii ni ile ya warajisi wa ushirika kunyamazia mapungufu ya kiutendaji katika ushirika na hivyo kusababisha yasifanyiwe kazi.
“Kiongozi mbadhirifu anatakiwa kuwajibishwa, lakini hatua zinazochukuliwa na warajisi dhidi ya viongozi wa ushirika kama wale waliosababisha upotevu wa pesa, mara nyingi hazisaidii kukomesha tabia hizo na mwisho wa siku vyama hufa,” alisema mkulima mdogo kutoka wilaya ya Kongwa, Dodoma, Kedimon Chilongola.
Chilongola anasema warajisi wamekuwa wakificha madhambi ya viongozi wa ushirika wasio waadilifu.
Kwa mujibu wa sheria, warajisi ndio wasimamizi wa sheria ya ushirika wakati ofisa ushirika wa wilaya ni mlezi. Sheria inataka mgogoro ufikishwe mahakamani pale tu mrajisi anapoona inafaa na kama hatua zote za kuusuluhisha zimechukuliwa.
Lakini wadau wanadai kwamba utatuzi wa migogoro hiyo haufanyiki kwa wakati na mara nyingi warajisi husimamia upande wa wabadhirifu na hivyo kuyaacha matatizo ya ushirika bila suluhu kitu ambacho huua ushirika.
Sera, sheria zibadilishwe
Joachim Simbachawene ambaye ni mkulima mdogo wa wilaya ya Mpapwa mkoani Dodoma anaamini kwamba kuna umuhimu wa sheria na sera za ushirika kubadilishwa kwa kuwa zimepitwa na wakati.
“Serikali imemuweka ofisa ushirika kama jicho la wanachama wasiokuwa na uwezo wa kubaini kinachoendelea. Ujue kwamba suala la fedha ni la kitaalamu. Sasa ofisa huyu yupo kwa ajili ya kutoa huo utaalamu. Anapoona kasoro inabidi aseme ili marekebisho yafanyike kwa maendeleo ya ushirika. Lakini kwa sababu ya ubadhirifu, hizi kasoro mara nyingi hazigunduliki na hivyo ushirika kufa,” anasema Simbachawene kwa masikitiko makubwa.
Simbachawene, ambaye kikundi chake cha ushirika cha Lumuma Saccos kilikufa mwaka 2015, anasema kuna haja ya kufanya mabadiliko katika uendeshaji wa ushirika.
Jeddidah Jere, ofisa ushirika kutoka Manispaa ya Morogoro na amabye alikuwepo wakati maoni ya wazalishaji wadogo yakitolewa dhidi yao, aliwasilisha mada kuhusu nafasi ya Serikali katika maendeleo ya ushirika.
“Wakati tukiwa hapa, tayari kuna juhudi za kuifanyia marekebisho sera ya sasa ya ushirika,” alisema Jere. Sera inayotumika kwa sasa ni Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002.
“Inatakiwa mambo yaende na wakati tuliopo ili baadhi ya malalamiko na lawama ambazo zimekuwa zikizungumzwa siweze kupungua au kuondolewa kabisa,” alisema Jere.
Nguli wa masuala ya maendeleo na sheria barani Afrika Profesa Issa Shivji anashauri kwamba ili kuufanya ushirika uweze kutoa mchango stahiki katika ujenzi wa uchumi mbadala ni ujenzi wa mfumo mpya wa ushirika nchini.
Ujenzi wa ushirika mpya
“Ni lazima ushirika ujengwe kutoka chini,” alisema Profesa Shivji wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika ofisini kwake wiki hii.
Tanzania imezoea kuenzi tamaduni za kikoloni za kutaka kudhibiti kila kitu, anasema Profesa Shivji na kuongeza: “Unapoleta taasisi na vyombo vya serikali (katika ushirika) vinakuja kwa lengo la kudhibiti. Haraka haraka taasisi hizo zinakuwa zana za udhibiti, siyo uwajibikaji.
“Hilo ndiyo tatizo. Usajili, kwa mfano, ni jambo la kikoloni. Unasajili magezeti, unasajili NGOs (mashirika yasiyo ya serikali), unasajili ushirika, kila kitu unataka kukisajili. Ukiangalia sheria zote hizi za usajili, mantiki yake ni udhibiti. Hili ni tatizo.
“Kadiri udhibiti unavyoongezeka, ndivyo rushwa navyo hushamiri. Sisemi kwamba kusiwe na udhibiti, lakini kwa nini watu wenyewe wasiruhusiwe kujidhibiti wenyewe? Kimsingi, hiyo ndiyo njia imara ya udhibiti.”
Nyamsenda, aliyetoa mada na kukabiliwa na maswali kutoka kwa wasikilizaji wake, hakujibu swali hata moja alipopanda jukwaani, pengine hakutaka kujifanya mtaalamu na kuwa na suluhu za kila tatizo. Aliwataka wazalishaji wadogo kutafakari namna wanavyoweza kutatua changamoto zao, akisisitiza kauli mbiu ya Mviwata ya “Mtetezi wa Mkulima ni Mkulima Mwenyewe”.
Lakini pembezoni mwa mkutano huo, Nyamsenda alilieza Mwananchi:
“Tunapaswa kufikiria ushirika mpya. Kunahitajika mabadiliko makubwa katika mfumo wa kiuendeshaji ambayo yataweka nguvu kwa wanachama, siyo serikali, kwa wanachama.
“Sasa mabadiliko haya hayatatokea kama zawadi. Ni mapambano.
Kwa sababu hata walioanzisha ushirika wa mwanzo, dola la kikoloni lilipinga na likaanza kuwakandamiza.
Lakini baadaye walipoona hilo vuguvugu limeshika nguvu wakataka kuliweka katika mbavu zao, na wakashindwa kufanya hivyo pia. Na nadhani huu ni wakati sahihi wa kufanya hivyo.”