Samia alivyowazungumzia wavamizi hifadhi za Taifa

Muktasari:
- Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema wale wote ambao watabainika kuvamia hifadhi za Taifa hawatovumilia na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Serengeti. Serikali ya Tanzania imesema haitamvumilia mtu yeyote atakayekiuka na kuvunja sheria za uhifadhi kwa kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo ya hifadhi za Taifa.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Desemba 23, 2019 na Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa) na Bonde Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Samia amesema Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha hifadhi hizo zinatunzwa na kuwa endelevu kwa manufaa ya Watanzania wote na kwamba jitihada hizo zinapaswa kuungwa mkono.
Amekemea tabia ya baadhi ya watu hususan viongozi kutumia mamlaka zao kuvunja sheria na kwamba Serikali haitasita kumchukulia hatua kali yoyote atakayekwenda kinyume cha sheria bila kujali cheo chake.
"Hapa naomba niongee na nyie wana Mara, unakuta kiongozi tena kiongozi wa chama tawala anavamia hifadhi halafu akiambiwa atoke anasema kuwa hatutoki, nasema kwamba hatutakuvumilia," amesema Samia
Amesema kizazi cha sasa kinapaswa kujifunza kuwa kizazi kilichopita ambacho kilifanikiwa kutunza hifadhi hizo hivyo kizazi hiki pia kina jukumu la kuhakikisha kinahifadhi hifadhi zilizopo kwaajili ya vizazi vijavyo.
Amesema katika kulinda na kuhifadhi wanyamapori, Serikali ya Tanzania imefanikiwa kudhibiti ujangili wa tembo katika hifadhi zake za Taifa kwa asilimia 90 baada ya kuwapo kwa ujangili uliokuwa ukitishia uhai na uwepo wa tembo katika hifadhi za Taifa.
Amesema Serikali itahakikisha inalinda wanyamapori na hifadhi ili kuwa sehemu ya urithi wa nchi na kwamba jamii inatakiwa kutoa ushirikiano ili kuweza kunufaika zaidi katika nyanja mbalimbali ikiwamo kiuchumi.