KUTOKA LONDON: Nilipokutana na Mwalimu Nyerere Brazil Juni 1991

Watu wengi hasa vijana wameniuliza ilikuwaje nilipokutana na Mwalimu Nyerere nikiishi Brazil, miaka 30 iliyopita.

Kabla ya kujibu ni vyema tukumbushane hali ilivyokuwa kipindi hicho.

Baada ya vita vikuu vya pili, dunia iligawanyika kifikra ubepari na ukomunisti (au usoshalisti, ujamaa, mrengo wa kushoto, nk). Mwalimu alikuwa msemaji na mpiganaji dhahiri wa ukombozi wa wanadamu. Alihesabika kuwa mrengo wa kushoto, ingawa sisi tulipenda kujiita nchi iliyokuwa na msimamo wa siasa isiyofungamana na upande wowote (non-aligned nations).

Kwa Waafrika Mwalimu alikuwa mstari wa mbele kusaidia vita dhidi ya ukoloni na kila Mtanzania anavyojua, wapigania uhuru na wakimbizi walipewa hifadhi hapa. Ndiyo maana matukio ya karibuni Afrika Kusini yanakinaisha! Kwa nyumbani Mwalimu aliongoza fikra za Ujamaa. Tuliitwa nchi ya kimaendeleo. Sasa Mwalimu aliongoza vita kumwondoa nduli Idi Amin wa Uganda na kuunga mkono jimbo la Biafra lilipojitenga na Nigeria, 1967. Alijihusisha na mengi ya kimataifa.

Ila kwetu Watanzania na hususani wanahabari tulimwogopa na kumheshimu.

Nilipoanza kazi ya uanahabari mwaka 1976, magazeti yalikuwa matatu tu, nchi nzima. Mfanyakazi la Jumamosi, Uhuru na Mzalendo la Tanu na hatimaye CCM. Kiingereza, Daily News, na dadake Jumapili yaani Sunday News. Miaka mitano baadaye nilikuwa mwanasafu wa Sunday News.

Kila gazeti lilikuwa na mhariri. Ila mhariri mkuu wa yote alikuwa Mwalimu Nyerere. Mwalimu alikuwa mwandishi mzuri. Tunavyojua alitafsiri vitabu viwili vya nguli William Shakespeare. Vitabu vya Mwingereza huyu ni vigumu, vimepevuka kilugha na kimaudhui,

Kijumla wanahabari tulikuwa makini sana.

Kuna wakati mwanahabari mmoja wa Uhuru aliandika habari kudunisha wakulima kijijini. Mwalimu aliwaita wahariri, akawagombesha na kuwakumbusha nafasi ya mwanahabari kuendeleza wananchi.

Miaka ya baadaye, mwalimu keshastaafu.

Mimi nimehamia Ughaibuni, huku bado nikituma habari na makala magazetini, nikisomea muziki Brazil. Nikaenda kumsikiliza Mwalimu akihutubia umoja wa watu weusi mjini Rio De Janeiro. Ilikuwa Juni 1991.

Kipindi hiki Mwalimu alihusika na maslahi ya watu wa nchi zinazoishi kusini ya dunia. Msimamo ule ule wa zamani.

Mfumo wa vyama vingi ulikuwa ukirindima barani baada ya kuanguka kwa himaya ya kikomunisti. Mwalimu akaulizwa nini msimamo wake, maana Tanzania ilikuwa na chama kimoja tu cha CCM kwa miaka mingi. Akajibu hatuwezi kuparamia tu mambo!

Mwalimu :“Demokrasia si kama chupa ya Cocacola...Siendi nchi fulani nikafikia hitimisho kuwa ina demokrasia kwa kuwa ina vyama vingi...” Baada ya hotuba iliyopigiwa vigelegele, mwenyeji wake Abdeas Nascimento, akasema Brazil ilikuwa na vyama vingi lakini uongozi uliodhalilisha maskini na hasa weusi. Vicheko. Baadaye ndipo nikakutana na Mwalimu uso kwa uso. Walinzi na wasaidizi wake wakatuzunguka. Baada ya shikamoo, akaniuliza, ninafanya nini huku? Haikuwa kawaida Watanzania kwenda Brazil.

Kwa karibu marehemu Nyerere alikuwa na umbo dogo sana (hakunizidi urefu) ila alikuwa na kitu kama nyota fulani iliyokusisimua ukiwa naye, akaonekana jabali. Si kwa majigambo au nyodo. Alikufanya ujihisi kama uko na rafiki yako wa siku nyingi mnaojuana toka utotoni.

Alitania tania na kugonganisha mikono.

Hiyo huitwa “charisma” kwa Kiingereza.

Binadamu hafundishwi huzaliwa nayo. Ukijumlisha hali hiyo na mapenzi yake kwa watu, kutoibia nchi yetu na kujenga majumba ya fahari (kama viongozi wenzake wengi waliopita au walio hai bado Afrika) kulimfanya mtu wa kipekee sana. Alipofariki hapa London 14 Oktoba, 1999, tulilipita jeneza lake kwa mshituko, huzuni na matumaini. Matumaini kuwa Kambarage kapandikiza mbegu ya kudumu kwa Watanzania. Haitakaa ioze!