Mwaka mmoja wa mfumo mpya elimu msingi bila wadau kuujua

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako (kushoto) akizungumza na Waziri Kivuli wa Wizara hiyo, Suzan Lyimo ndani ya Ukumbi wa Bunge Dodoma, baada ya kuwasilisha bungeni bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17. Picha na Maktaba.
Moshi. Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imetoa mtalaa mpya wa elimu ya msingi ambao utatekelezwa katika kipindi cha miaka saba huku baadhi ya wadau wa elimu wakisema hawaufahamu.
Lengo la mtalaa huo ambao umeanza kutumika mwaka huu, ni kuwawezesha wahitimu kushiriki kikamilifu katika jitihada za Serikali kuwezesha uchumi wa nchi kukua na kufikia uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025.
Mtalaa huo umejikita kuimarisha kusoma, kuandika na kuhesabu katika madarasa mawili ya kwanza, mambo ambayo katika miaka ya karibuni yameonekana kukosekana hata kwa wanafunzi wanaomaliza elimu ya sekondari ambao baadhi, licha ya kufaulu, walikutwa wakiwa hawajui kusoma.
Mkurugenzi mkuu wa TET, Dk Aneth Komba amesema katika maelezo yake kuwa mitalaa itaendelea kuboreshwa sambamba na mabadiliko yanayotokea kila baada ya mzunguko mmoja wa wahitimu.
Alisema TET, kwa niaba ya Wizara ya Elimu, iko tayari kupokea maoni ya kuboresha mtalaa huo kutoka kwa walimu na wadau wengine.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, malengo mengine ni kumuandaa mwanafunzi kukabili mazingira yake na kushiriki katika kuchangia maendeleo na uchumi wa kati wa viwanda.
“Mtalaa umelenga kumjengea mwanafunzi uzoefu mpana wa kujifunza na unasisitiza matumizi ya mbinu shirikishi za kufundishia na kujifunzia zinazogusa mahitaji ya kila mwanafunzi,” alisema.
“Msisitizo upo katika kumjenga mwanafunzi katika nyanja zote za kujifunza kiroho, kimaadili, kiakili, kimwili na kijamii,” alisema Dk Komba katika ujumbe ulioambatanishwa na mtalaa huo.
“Ni matumaini yangu maudhui ya mtalaa huu yatawaongoza watekelezaji kutumia fursa walizonazo kumwezesha mwanafunzi kujenga umahiri utakaomsaidia kuyamudu maisha yake katika jamii.
“Ili kubaini kiwango cha mafanikio katika kujifunza, upimaji utafanyika kwa kuzingatia uwezo wa mwanafunzi kutenda na uwezo wake katika kujipima mwenyewe,” alisema Dk Komba.
Kaimu Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Lyabwene Mtahabwa aliithibitishia Mwananchi jana kutolewa kwa mtalaa huo na kueleza kuwa umeanza kutumika 2019.
“Kama ni mtaala wetu tumeusaini, basi unaambatana na barua ya lini unaanza kutumika. Huo unaousema tumesambaza Zanzibar na Bara na maofisa elimu wote wanajua,” alisema Dk Mtahabwa.
Katika maelezo ya utangulizi katika mtalaa huo, Dk Mtahabwa anasema umegawanyika katika sehemu kuu mbili, yaani darasa la kwanza hadi la pili na sehemu ya pili ni darasa la tatu hadi la saba.
Kwa mujibu wa Dk Mtahabwa, sehemu ya kwanza mtalaa umejikita katika kumjengea mwanafunzi umahiri katika stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).
“Sehemu hii imeandaliwa kwa kuzingatia kwamba miaka ya mwanzo ya kujifunza ni muhimu sana katika makuzi ya mtoto kiakili, kimwili na kijamii,” anasema Dk Mtahabwa.
Dk Mtahabwa alisema maudhui ya sehemu ya pili yameandaliwa katika mtindo wa kukuza umahiri katika masomo manane yakiwamo Kiswahili na Kiingereza.
Masomo mengine katika sehemu hiyo ya pili ni hisabati, uraia na maadili, sayansi na teknolojia, maarifa ya jamii, stadi za kazi na masomo chaguzi ya lugha ya Kifaransa na Kiarabu.
Hata hivyo, katika sehemu hiyo, umahiri wa KKK unaendelea kupewa msisitizo katika masomo kwa sababu ni msingi muhimu katika kumwezesha mwanafunzi kujifunza masomo kwa ufanisi.
Mambo yaliyozingatiwa
Mtalaa huo umezingatia kuwa elimu ya msingi itakuwa ni ya miaka saba ili kufikia umahiri uliokusudiwa.
Kwa mujibu wa andiko hilo, mtalaa huo unalenga kuendeleza umahiri uliojengwa na mwanafunzi kutoka darasa moja kwenda jingine.
“Hivyo, katika kila darasa kutakuwa na kukazia ujuzi na maarifa kwa yale ambayo mwanafunzi amejifunza madarasa la nyuma.
“Muhimu ni kwamba kutakuwepo na ufuatiliaji wa karibu wa utendaji wa mwanafunzi katika kila darasa ili ajenge umahiri uliokusudiwa,” anasisitiza katika maelezo hayo.
Mtalaa vilevile umeandaliwa kwa kuzingatia Sheria ya Elimu, matamko ya kisera, na mengine ya kitaifa na kimataifa.
Muda wa kufundisha
Kwa mujibu wa mtalaa huo, mwaka wa shule utakuwa na siku 194 ambazo ni sawa na wiki 39, ukiwa umegawanywa katika mihula miwili ya masomo.
Katika kila muhula wiki mbili zitatumika kwa upimaji na ili kufikia malengo ya mtalaa na kupata matokeo yanayotarajiwa, mwanafunzi wa madarasa mawili ya kwanza atasoma stadi sita ambazo ni kusoma, kuandika, kuhesabu, kutunza afya na mazingira, kujiendeleza kimichezo na sanaa pamoja na elimu ya dini na muda wa kufundisha kwa wiki ni saa 15 zlizogawanywa kwa vipindi sita kwa siku.
Muda wa kila kipindi utakuwa wa dakika 30, hivyo katika siku moja ya mafunzo itampasa mwanafunzi kujifunza kwa muda wa saa tatu tu.
Mgawanyo huo wa muda unaonyesha kwamba eneo la KKK linachukua asilimia 80, eneo la stadi wezeshi ( 13) na elimu ya dini (7) ya muda wote.
Wasemacho wadau
Mwananchi ilizungumza na wadau wa elimu ambao walikuwa na mitazamo tofauti huku wengine wakidai hawaufahamu.
Wilfred Mauki ambaye ni mwalimu kitaaluma, alisema mtalaa huo ni tofauti na mitalaa ya 2015 na 2016, lakini umeleta mkanganyiko katika muda wa kumaliza elimu ya msingi.
“Lengo kuu la mtalaa huu ni kumuandaa mwanafunzi kuwa mahiri katika kujifunza na kukazia ujuzi na maarifa aliyojifunza, tofauti na mitaala iliyopita,” alisema.
“Mitalaa ya mwaka 2015 na 2016 ilijikita katika kuimarisha maarifa katika ngazi ya elimu ya msingi ambayo ilikuwa inaishia darasa la sita; hii (2019) inaishia la saba,” alisema.
Hivyo ni dhahiri mtalaa huu umeleta mkanganyiko katika jamii kuwa elimu ya msingi ni miaka saba tofauti na sera ya elimu mwaka 2014, kuwa elimu msingi ni miaka kumi.”
Mkanganyiko mwingine ni sera ipi hasa inayotumika kuendesha elimu kwa mujibu wa utangulizi kwenye sera ya 2014 ni dhahiri sera ya elimu ya mwaka 1995 ilishafutwa kwa sera hii,” alisema.
Anataja mkanganyiko mwingine ni kutokuwa na falsafa ya elimu inayoendana na sera zinazotumika sasa ya mwaka 1995 na 2014 hivyo bado Tanzania inatumia falsafa ya elimu ya kujitegemea ya 1967 .
Hata hivyo, ametaja faida za mtalaa wa Elimu ya Msingi wa mwaka 2019 kuwa unamwezesha mwanafunzi kujenga umahiri wa kusoma, kuandika na kuhesabu kuanzia darasa la I na la II.
“Ni eneo ambalo liliachwa na mitaala mingine na kupelekea kuzalisha wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika shule za sekondari,” alisema.
“Mtaala huu umejikita katika umahiri ambao utamwezesha mwanafunzi wa darasa la tatu hadi la saba kuwasiliana kwa ufasaha kwa Kiswahili na Kiingereza kwa kuzungumza na kuandika,” alisema.
“Mabadiliko mengine yametokea kwenye idadi ya vipindi, mitaala ya 2015 na 2016 ilikuwa na idadi chache ya vipindi ukilinganisha na mtaala wa 2019,” aliongeza.
Mtendaji mkuu wa Taasisi ya Ubunifu Tanzania (EIT), Benjamin Nkonya alisema ndio kwanza anasikia uwepo wa mtalaa huo mpya, lakini kwake anachoangalia ni nini mhitimu anatoka nacho.
“Ndio kwanza nasikia kutoka kwako ila nataka niseme tunaweza kuwa na mitaala mizuri sana au vitabu vizuri sana lakini matokeo ya kujifunza ndio ya ninayoangalia.
“Tunataaka kuona mitaala inayowaandaa Watanzania kushindana katika soko la ajira na kusimamia rasilimali zetu. Kama hautufikishi huko, hiyo ni pombe ya zamani inawekwa kwenye chupa mpya,”.
Waziri Kivuli wa Elimu, Susan Lyimo (Chadema) alisema hana taarifa juu ya mtalaa huo wa 2019 bali anachofahamu ni mtalaa wa 2016 lakini akasema alijua kuna kitu kama hicho kingekuja 2019.
“Aim not aware (sifahamu) lakini nilijua kitu kama hicho kitakuja. Wametunga sera ambayo inasema elimu msingi ni elimu ya awali hadi kidato cha nne ukiondoa darasa la saba,” alisema Lyimo.
Hata hivyo, Lyimo ambaye ni mbunge wa viti maalumu, alisema Serikali imeshindwa kuitekeleza kwa sababu hakuna miundombinu wala walimu.