Jinsi mchakato wa kumng’oa Trump utakavyokuwa

Muktasari:
Rais Trump amwandikia barua ya hasira Spika Nancy Pelosi.
Washington, Marekani. Bunge la Marekani limepiga kura ya mchakato wa kumng’oa madarakani Rais wa Donald Trump.
Matokeo ya kura hiyo yanatarajiwa kutolewa leo ambako itaamua endapo kiongozi huyo ataendelea kubaki madarakani au la.
Baada ya kura kupigwa, endapo wajumbe wa Bunge la Wawakilishi wanaounga mkono Rais Trump aondolewe madarakani watakuwa chini ya nusu, Rais huyo ataendelea na madaraka yake. Ikiwa watakuwa zaidi ya nusu au asilimia 51 atakuwa ameondolewa.
Baada ya hatua hiyo, mashtaka dhidi yake yatapelekwa katika Seneti.
Baada ya mashtaka kusikilizwa, Seneti nayo itapiga kura kuamua kama Trump ana hatia au la.
Katika matokeo ya kura ya seneti, ikiwa zaidi ya nusu watasema hana hatia, Trump ataendelea na madaraka yake na ikiwa theluthi watasema ana hatia, Trump atapoteza urais na makamu wake atachukua nafasi.
Wakati Bunge la wawakilishi lina wajumbe wengi wa Democrats, Seneti inatawaliwa na wajumbe wengi kutoka chama cha Republican cha Rais Trump.
Katika hatua nyingine, Rais Trump amekosoa uamuzi wa kufanya uchunguzi dhidi yake na kudai kuwa Spika Nancy Pelosi ametangaza vita.
Rais Trump alimuandikia barua Spika wa Pelosi akikosoa hatua ya uchunguzi dhidi yake.
Aidha, Rais huyo alisema spika Pelosi ametangaza vita ya wazi dhidi ya demokrasia ya Marekani.
“Umelishushia hadhi na umuhimu wa neno uchunguzi,” alisema Rais Trump kupitia barua yake iliyotumwa kwa spika Pelosi juzi Jumanne 17.
Rais Trump anatuhumiwa kuishikiza Ukraine kuvuruga Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Katika barua hiyo yenye kurasa sita, Rais Trump alionyesha hasira zake dhidi ya mchakato na kumpinga Pelosi anayetoka chama cha upinzani cha Democrats.
Kupitia barua hiyo, Trump anadai alinyimwa haki ya kimsingi ya kikatiba kuanzia mwanzoni mwa mchakato huo wa uchunguzi ikiwamo kuwasilisha ushahidi.
“Umeshushia hadhi umuhimu wa neno Uchunguzi!” aliandika katika barua iliyotumwa Jumanne…Haki ya mchakato ilitolewa zaidi kwa wale walioshtaki katika kesi za ‘Salem Witch Trials’ (kesi za kusaka wachawi),” aliandika Trump.
Kesi za “Salem Witch Trials” zilifunguliwa kati ya Februari 1692 na Mei 1693 huku Massachusetts, Marekani. Watu zaidi ya 200 walishtakiwa, 30 kati yao walipatikana na hatia na 18 kati yao waliuawa kwa kunyongwa.
Madai hayo ya Trump yamekuja wakati ambako kiongozi huyo alialikwa na mwenyekiti wa Kamati ya Sheria ya Bunge, ambayo ilikuwa ikikusanya ushahidi huo ili kutoa ushahidi wake lakini kiongozi huyo alikataa.