Salamu za Zitto kwa wafanyakazi Mei Mosi

Muktasari:

Amesema Wafanyakazi kwenye sekta rasmi wanaofikia 2.1 milioni ni jeshi kubwa la kuleta mabadiliko nchini kwetu.


Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ametuma salamu za sikukuu ya wafanyakazi ya Mei Mosi leo, akiwataka wanaharakati kupaza sauti kupigania haki za wafanyakazi.

“Tunatuma salamu za mshikamano kwa tabaka la wafanyakazi nchini katika siku hii muhimu kwao. Wafanyakazi kwenye sekta rasmi wanaofikia 2.1 milioni ni jeshi kubwa la kuleta mabadiliko nchini kwetu. Tutimize wajibu huo,” amesema Zitto.

Kadhalika, mwanasiasa huyo ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini amesema wafanyakazi wanaumizwa na mzigo wa kodi kwa sababu hawana fursa za kuukwepa  kisheria.

Amesema kodi kwa wafanyakazi hukatwa moja kwa moja kutoka kwenye mishahara yao tofauti na wenye mitaji ambao kuna wakati huweza kuzikwepa au kujadiliana na mamlaka husika namna ya kuzilipa.