Zitto amlilia Lissu ACT ikimomonyoka

Muktasari:

  • Hata hivyo, chama hicho kimesema licha ya jana kuondokewa na wanachama 10 akiwamo mjumbe wa kamati kuu, Samson Mwigamba bado kitabaki kuwa imara.

Dar es Salaam. Wakati kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akiandika waraka kwa Tundu Lissu, chama chake kimezidi ‘kubomoka’ kwa wanachama wake kukimbilia CCM.

Hata hivyo, chama hicho kimesema licha ya jana kuondokewa na wanachama 10 akiwamo mjumbe wa kamati kuu, Samson Mwigamba bado kitabaki kuwa imara.

Jana, Zitto aliandika kuwa amefarijika kusikia kauli ya Lissu na kumweleza kuwa Watanzania wamefarijika kwamba bado yuko hai na ataweza kuungana nao kuendeleza mapambano ya kujenga demokrasia.

“Siku ile nimekuja kukusabahi uliniuliza nini kinaendelea nyumbani. Nilikwambia tu Watanzania wanakuombea. Ukanitazama kwa lile jicho lako la ki-Marx, ukacheka na kusema ‘Taifa la waomba Mungu’. Tukacheka. Ni kweli Watanzania wamekuombea sana, na ni jambo la kushukuru kuwa Mola amewasikiliza maombi yao,” aliandika Zitto kwenye waraka huo.

“Nina furaha kuwa unaendelea vizuri sana tofauti na nilipokuja kukuona. Tutazidi kumwomba Mola afya yako iimarike zaidi. Tuna kazi kubwa sana mbele ya safari na kwa hakika ni lazima tuifanye kwani tusipoifanya nchi yetu itaanguka kiuchumi na kidemokrasia, na watu wetu kuendelea kuwa maskini zaidi kuliko ilivyo sasa.”

Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini aliendelea kumwandikia Lissu kuwa ilikuwa ni lengo la waliomshambulia kuwanyamazisha, lakini anawaeleza hawatanyamaza kamwe.

Alienda mbali zaidi na kumwambia Lissu, “Wewe umetuonyesha hilo kwa vitendo na ndio maana upo hospitali Nairobi. Sisi sote twapaswa kuwa Tundu Lissu.”

Hata hivyo, wakati Zitto akiandika waraka huo upande wa chama chake umeendelea kukumbwa na misukosuko baada ya jana Mwigamba kuwaambia waandishi wa habari kwamba baada ya kutafakari kwa kina ameamua pamoja na wanachama wengine kukihama chama hicho.

Alizitaja sababu za kuhamia CCM kuwa ndiyo chama kinachoakisi kwa karibu itikadi, falsafa na sera za ACT Wazalendo.

Mwigamba alisema wamefanya hivyo ili kujiunga katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.

Alisema kilichowasukuma ni kutokana na kufuata misingi ya Azimio la Tabora ambayo kwa kiasi kikubwa CCM inayatekeleza.

Aliitaja sababu nyingine kuwa ni kujitenga na upinzani unaokerwa na mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano.

“Baada ya kutangaza kujivua uongozi baadhi ya viongozi wa ndani ya chama waligeuka vichaa wakinitukana kila aina ya matusi.

“Cha ajabu hata wale wanaofahamu na kuitetea misingi ya chama walitukanwa na viongozi wakiwapo tena wa ngazi za juu na wamekaa kimya, hii inaonyesha wamewatuma,” alisema Mwigamba.

Aliongeza kuwa uamuzi huo umekuja kufuatia kushuhudia uongozi wa sasa wa ACT Wazalendo ‘ukichepuka’ kwa kasi na kuacha misingi ya chama jambo ambalo ni kinyume cha katiba ya chama hicho.

Mwigamba alifafanua kuwa amevumilia mengi ikiwamo kushuhudia wafuasi wa watu wakipewa uongozi ukiwa ni mwendelezo wa matatizo yaliyoanza baada ya Uchaguzi Mkuu ndani ya chama mwaka 2015, ambapo kulikuwa na ombwe la wafuasi wa watu ambao walionekana wanajua siasa.

Alisema kwamba wafuasi hao ndiyo wamekuwa na thamani kuliko walioteseka, akiwamo yeye aliyedai kulala kwenye sakafu ya chama makao makuu ili kukijenga.

“Wengine wanaendelea kula posho za ubunge ambao leo wao ndiyo wanachama na sisi ni wasaliti, ” alisema Mwigamba.

Hata hivyo, chama hicho kimeeleza kwamba hata kabla hajaamua kujivua uanachama, tayari alikuwa ameondoka kwenye nafasi zote muhimu na kubaki mwanachama wa kawaida, lakini chama kilibaki imara.

Kauli ya chama hicho ilikuja kufuatia kuondoka kwake pamoja na wanachama 10 waliotangaza kujiunga na CCM.

Akizungumzia suala hilo, katibu mkuu wa ACT Wazalendo, Doroth Shamu alisema chama hakitatetereka kwa sababu walioondoka walishindwa kutumia nafasi zao kutoa maoni kwa lengo la kuboresha badala yake walifanya hivyo kuvuruga.

Alisema manung’uniko nje ya utaratibu ni usaliti na si utendaji na kwamba Mwigamba angekuwa mzalendo na ana uchungu na chama kama anavyojinasibu angefuata katiba ya chama.