Zimamoto wataka visima vya maji

Muktasari:

  • Ombi hilo lilitolewa jana na Kamanda wa Zimamoto Morogoro, Ramadhani Pilipili wakati akizungumza kuhusu changamoto zinazolikabili jeshi hilo.

Morogoro. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro limeiomba Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kukarabati na kujenga visima zaidi ya 80 vya kuchota maji yanayotumika kuzima moto.

Ombi hilo lilitolewa jana na Kamanda wa Zimamoto Morogoro, Ramadhani Pilipili wakati akizungumza kuhusu changamoto zinazolikabili jeshi hilo.

Pilipili alisema miaka ya zamani kila mtaa Manispaa ya Morogoro kulikuwa na kisima cha kujaza maji kwenye magari ya kuzimia moto lakini kwa sasa kimebaki kimoja.

Pia, alisema kutokuwapo visima vya kutosha, kunaifanya kazi ya uzimaji moto kuchukua muda mrefu kutokana na waokoaji kutembea umbali mrefu kwenda kujaza maji kwenye kisima kilichopo maeneo ya Forest ambacho ndicho kina uhakika wa kutoa maji.

Kamanda Pilipili alisema mwaka jana ofisi yake ilishawasilisha maombi kwa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Morogoro (Moruwasa) ya kukarabatiwa visima 69 lakini hadi sasa hakuna hata kimoja kilichokarabatiwa.

Meneja ufundi wa Moruwasa, Halima Mbiru alisema kuwa kwa muda mrefu visima hivyo havijafanyiwa ukarabati kutokana na ufinyu wa bajeti.