Waziri wa Fedha Z’bar atishia kusitisha mkataba wa ujenzi

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Khalid Salum Mohammed


Muktasari:

Serikali haitakuwa tayari kuona makubaliano yaliyopo kati yake na Kampuni ya Dezo hayatekelezwi

Zanzibar. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Khalid Salum Mohammed ametishia kusitisha mkataba wa ujenzi na Kampuni ya Dezo Civil Contractors Co Limited inayojenga nyumba za maendeleo zilizo chini ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), endapo itashindwa kutekeleza majukumu yake kwa wakati.

Alisema makandarasi wakishindwa kujenga nyumba hizo kwa mujibu wa makubaliano, Serikali haitosita kuchukua hatua ikiwamo kuwatafuta wengine na kuachana na kampuni hiyo.

Dk Mohamed alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na uongozi wa kampuni hiyo katika ziara ya kuangalia hatua zilizofikiwa na miradi inayosimamiwa na ZSSF maeneo ya Michenzani, Darajani na Mbweni.

“Serikali imepanga mipango ya kimaendeleo ikiwamo ujenzi wa miradi ya nyumba hizo, hivyo haitakuwa tayari kuona makubaliano yaliyopo kati yake na kampuni husika hayatekelezwi kama ilivyotarajiwa,” alisema Dk Mohamed.

Alisema utekelezaji mzuri wa miradi hiyo utasaidia kufikia malengo ya dira ya maendeleo ya mwaka 2020 na ukuzaji uchumi kwa mwaka wa fedha 2018/19 kupitia sekta zake za ukusanyaji wa mapato visiwani hapa.

Dk Mohamed alisema Serikali kupitia ZSSF, imetenga Sh43.7 bilioni kwa ajili ya mradi huo na haitasita kufanya ziara za mara kwa mara katika miradi hiyo ili kuona ndani ya mwaka huu baadhi ya majengo yamekamilika.

Hata hivyo, mkandarasi wa kampuni hiyo, Hitest Thaller alisema pamoja na kuwapo kasoro za kiutalaamu wataongeza kasi ya ujenzi ili kuhakikisha ndani ya mwaka huu wanaanza kukabidhi nyumba hizo.

“Mheshimiwa waziri nikihakikishie kuwa tumejipanga vyema kikazi mimi na timu yangu yote na tunaahidi ndani ya mwaka huu tutakabidhi nyumba kama tulivyokubaliana,” alisema Thaller.

Kaimu meneja wa ZSSF, Abdul-Azizi Ibrahim Iddi alisema katika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kama ilivyokusudiwa, taasisi hiyo itatumia timu yao ya wataalamu kufuatilia hatua kwa hatua hadi ujenzi ukamilike kwa wakati.