Waziri Ummy Mwalimu awapa ukomo TFDA

Muktasari:
- TPSF yatoa changamoto tano
Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameitaka Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), isichukue zaidi ya siku 10 kutoa usajili kwa viwanda vya chakula na siku 30 kutoa majibu ya ubora wa bidhaa.
Amesema agizo hilo ni katika mikakati ya kuondoa kasoro zote za uanzishwaji wa viwanda vya bidhaa za chakula nchini, katika kufikia nchi ya uchumi wa viwanda 2025.
Ummy ameyasema hayo leo Julai 30, 2018 wakati akijibu hoja kwenye mkutano wa wadau kujadili mchango wa taasisi za Serikali katika kuanzisha na kuboresha viwanda vya chakula nchini.
"Usajili usichukue zaidi ya siku 10, naagiza nataka ndani ya siku 30 muwe mmeshatoa majibu au taarifa kuhusu bidhaa husika watu wasisubiri sana, lakini pia muanze kutoa mafunzo kwa wasindikaji wa chakula. Fanyeni kazi na chuo kikuu cha Sokoine SUA ili kuzalisha wataalamu zaidi," amesema Waziri Ummy.
Awali, akiwasilisha mada, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye ametoa changamoto tano zinazowakumba wazalishaji wa bidhaa za chakula nchini.
Amesema licha ya wadau kupunguza malalamiko bado kuna changamoto ndani ya sekta ikiwemo miundombinu sahihi.
"Bado hakuna miundombinu iliyoandaliwa kiafya, kimazingira na ile inayofuata sheria,” amesema.
“Tunaangalia sekta binafsi tunachangia kivipi kutatua tatizo hili bado hatujafikia utatuzi, bado wawekezaji wanahangaika kupata maeneo ambayo yameandaliwa na yapo tayari kwa uwekezaji."
Ameitaja changamoto ya pili ni uhaba wa mafunzo na elimu inayotakiwa kuwekezwa kuwa bado havijafika.
"Changamoto ya tatu ni ubora wa malighafi kutoka katika sekta ya kilimo kwani inayokwenda viwandani haina ubora wa kutosha katika viwanda,” amesema.
“Nne, ucheleweshwaji wa kufanya tathmini baada ya kupokea maombi bado muda ni mrefu sana bado hamjafikia kiwango ambacho tunataka muende nacho katika awamu hii ya tano."
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Agnes Kijo amesema mamlaka hiyo ineweza kubadili mfumo wake na imeendelea kurahisisha huduma.
"Tumeendelea kurahisisha huduma na tumebadilisha mfumo kuwa wa kielektroniki, tumeongea muda wa kutoa huduma mpaka siku za Jumamosi ili kuhakikisha tunafikia lengo kwani ni hatua mojawapo ya kuleta mabadiliko katika uchumi wa viwanda," amesema Kijo.