Wanaume Kanda ya Ziwa waanikwa

Muktasari:

Imeelezwa asilimia 56 ya kaya wilayani hapa zinakabiliwa na umaskini na njaa kila mwaka kutokana na vitendo hivyo.

Sengerema. Tabia ya wanaume wilayani hapa, Mkoa wa Mwanza kuuza mazao yakiwa shambani au yaliyohifadhiwa nyumbani bila kuwashirikisha wenzi wao imedaiwa kuchangia umaskini na njaa.

Imeelezwa asilimia 56 ya kaya wilayani hapa zinakabiliwa na umaskini na njaa kila mwaka kutokana na vitendo hivyo.

Hayo yalibainika wakati wa mdahalo ulioandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Kivulini kujadili changamoto zinazosababisha umasikini wa kipato na njaa miongoni mwa wakazi  wilayani hapa.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Yassin Ally alisema utafiti kuhusu umaskini wa kipato na tatizo la njaa kwa Sengerema umebaini familia nyingi hupata mavuno ya kutosha kutokana na kilimo cha mahindi na mpunga, lakini mazao hayo huuzwa na wanaume yakiwa shambani au baada ya kuvunwa na kuhifadhiwa nyumbani.