Wajumbe 40 wa serikali za mitaa wapewa mafunzo kufuatilia maji

Muktasari:

Wakazi wa maeneo hayo wanatumia maji ya visima na yale yanayosambazwa kwenye magari.


Dar es Salaam. Wajumbe 40 wa serikali za mitaa kutoka kata tatu za Chanika, Buyuni na Msongola wamepewa mafunzo maalum ya kuanzisha na kufuatiliaji kamati za maji kwenye mitaa yao isiyokuwa na kamati hizo ili kuharakisha upatikanaji wa maji.

Mafunzo hayo yametolewa na Shirika la Upendo Community linalotekeleza mradi wa ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma katika sekta ya maji kwenye kata tatu za mradi zilizopo pembezoni mwa Manispaa ya Ilala.

Kata hizo ni za maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya maji kwa sababu hayajaunganishwa na mtandao wa maji wa Dawasco.

Wakazi wa maeneo hayo wanatumia maji ya visima na yale yanayosambazwa kwenye magari.

Akizungumzia mafunzo hayo jana, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chanika, Ashery Mtemi alisema ameridhishwa na mafunzo hayo ambayo yanahamasisha ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma hasa katika sekta ya maji na kuwataka wajumbe wakasimamie ukusanyaji wa mapato kwenye maeneo yao.

“Kamati hizi za maji ni muhimu kwa sababu zinaongeza hamasa na msukumo wa kuwaletea wananchi uhakika wa maji. Nina imani wajumbe hawa sasa wanajua wajibu wao na nini cha kufanya kwenye kamati hizo,” alisema.

Mratibu wa mradi huo, Victoria Innocent alisema kabla ya mradi kutekelezwa, baadhi ya mitaa haikuwa na kamati za maji, mitaa mingine  haikuwa na akaunti benki za kuhifadhia fedha, pia taarifa za mapato na matumizi zilikuwa haziwekwi kwenye mbao za matangazo na kusomwa kwenye vikao vya wanachi.

Alisema kwa sasa kata hizo zimepiga hatua kwa sababu zimefungua akaunti benki, kwa mfano katika mitaa ya Vikongoro, Ngwale, Lukooni na kitonga. Pia, alisema taarifa za mapato na matumizi zinatolewa kwa wanachi na huduma za maji zimeboreshwa.

"Kutokana na zoezi hili, ni dhahiri sasa wenyeviti wa mitaa watahimiza wananchi kulipa kodi kwa uaminifu katika mitaa yao ili kuweza kutumika katika kutatua baadhi ya changamoto katika sekta majo kwenye katetu,"alisema.